Na Benjamin Madaha
WAFANYABIASHARA, waajiriwa na vijana wanaojitafuta – kuna ukweli mgumu kidogo kwenye elimu ya fedha ambao watu wengi hawafundishwi. Akaunti yako ya kuhifadhi (savings) haikuokoi wewe. Inaiokoa benki.
Benki kama X Bank, Y Bank na T Bank Tanzania zinapenda sana watu kuweka pesa zao kwenye ‘savings’. Kwa nini? Kwa sababu benki hutumia pesa zako kuzikopesha kwa wengine kwa riba kubwa zaidi.
Mfano rahisi; unaweka pesa, benki inakupa interest (riba) ya asilimia 1. Benki inakopesha watu kwa 18% – 20%. Tofauti hiyo ndiyo biashara ya benki.
Lakini, kuna kitu kingine hatari zaidi kinaitwa mfumuko wa bei (Inflation). Inflation inakula pesa zako polepole. Tuseme inflation kwa Tanzania iko karibu 3.5% kwa mwaka.
Lakini savings account inakupa riba ya 1%. Maana yake nini? Kila mwaka nguvu ya pesa yako inapungua. Mfano; unaweka 10,000,000 benki, inakupa 1% lakini inflation inakula 3.5%.
Hivyo, pesa yako kiuhalisia inapungua thamani. Unafikiri una-save… lakini kwa uchumi halisi unapoteza nguvu ya pesa.
Savings ni kwa usalama, sio utajiri. Savings account ina kazi moja muhimu. Ni kwa ajili ya ‘Emergency fund’, inapaswa kukusaidia kwa dharura, hospitali, ajali au miezi michache utakayokuwa huna kipato. Sio mahali pa kujenga utajiri.
Matajiri hutumia benki tofauti na watu wengi. Watu wengi wanafikiri matajiri wana pesa nyingi benki. Ukweli ni tofauti.
Matajiri hutumia benki kukopa, hutumia pesa kuwekeza na hutumia ‘leverage’. Benki kwao ni ‘tool’ (zana) na sio mahali pa kuficha pesa.
Swali ni je; kama si savings, basi pesa iwekwe wapi? Assets zinazozalisha pesa kama nyumba za kupangisha, mashamba ya biashara au biashara inayouza kila siku. Hizi assets zinaweza kuongeza kipato kila mwezi.
Pia, kuna biashara yenye ‘cashflow’ ya kila siku. Hii ni muhimu sana Afrika. Biashara zinazofanya vizuri sana ni usambazaji wa chakula, maji, ‘transport’ (usafiri), vifaa vya ujenzi, n.k.
Vilevile, kuna ‘skills’ zinazouzwa sokoni. Ujuzi kama masoko, mauzo na ushauri. Hizi zinaweza kukuingizia pesa bila mtaji mkubwa.
Je, ni mfumo upi mzuri wa pesa? Watu wanaofanikiwa kifedha mara nyingi wana mfumo huu; 10–20% (akiba), 40–60% (uwekezaji/biashara), 20-30% (matumizi ya maisha).
Kosa kubwa la watu wengi ni kuweka akiba ya fedha nyingi, huku wakiwa hawawekezi wala hawana asset. Hapo ndipo wanapochelewa kutoboa.
Mwisho, benki sio adui lakini sio njia ya kutajirika. Benki ni sehemu ya kuhifadhi pesa kwa muda na kupata mikopo. Utajiri hujengwa kwenye assets.
Mwalimu Benjamin Madaha ni mchambuzi mbobezi wa masuala ya elimu ya fedha.


