MOSCOW, Urusi
MAMLAKA nchini Urusi zimetangaza kuwashikilia watu watatu wanaohisiwa kuhusika katika mauaji ya aliyekuwa kiongozi wa juu wa jeshi, Luteni Jenerali Vladimir Alexeyev.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Uchunguzi (SK), moja ya waliotiwa mkononi ni raia wa Urusi mzaliwa wa Ukraine, Lyubomir Korba.

Inaelezwa kuwa Korba aliingia Urusi mwishoni mwa mwaka 2025 akiwa ametumwa na vyombo vya usalama vya Ukraine kwenda kutekeleza shambulio la kigaidi la kumuua kiongozi huyo mwandamizi wa jeshi.
Alexeyev (64), alishambuliwa akiwa nyumbani kwake Kaskazini-Magharibi mwa Moscow na alifariki akiwa hospitali alikopelekwa kwa matibabu.
Inafahamika kuwa Alexeyev alikuwa kiongozi wa pili kimamlaka katika Idara ya Usalama wa Taifa ya Urusi. Ni mwendelezo wa viongozi wa jeshi la nchi hiyo kushambulia tangu walipovamia Ukraine mwaka 2022.
Hata hivyo, mamlaka za Ukraine zimeendelea kusisitiza kuwa hazijahusika katika shambulio lililoondoa uhai wa Alexeyev.


