Na Winfrida Mtoi, Gazetini
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema kuwa muda wowote, kocha Miguel Gamondi atasaini rasmi mkataba wa kuifundisha timu ya taifa ya soka ya Tanzania, Taifa Stars na malipo yake yote yatagharamiwa na Serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam leo Februari 9, 2026, Makonda amesema Gamondi amestahili mkataba huo baada ya kuonyesha uwezo wa hali ya juu katika michuano ya AFCON iliyofanyika Morocco.
Ameeleza kuwa makocha wengi wametuma CV za maombi ya kuinoa timu hiyo lakini wameona wabaki na mwalimu ambaye yatari amefanya kazi nzuri na amewajua wachezaji.
“Upande wa Serikali wameshamaliza, BMT na TFF wameshamaliza, kazi iliyobaki ni yeye na ajenti wake wakamilishe utaratibu. Serikali chini ya Rais wetu Dk. Samia Suluhu Hassani ndiye aliyebeba jukumu la kulimpa kocha,”
Gamondi aliiongoza Taifa Stars kufika hatua ya 16 ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania akiwa kocha wa muda., endapo atasaini mkataba huo, ataiongoza Taifa Stars katika michuano ya AFCON 2027, ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji.


