PRETORIA, Afrika Kusini
SERIKALI ya Afrika Kusini imetangaza kuwarudisha nyumbani wanajeshi wake waliokuwa kwenye operesheni ya kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Ikumbukwe, wanajeshi hao walikuwa chini ya mwamvuli wa programu ya Umoja wa Mataifa ya kulinda amani (MONUSCO) katika Taifa hilo.
Afrika Kusini imekuwa sehemu ya operesheni huyo ya Umoja wa Mataifa kwa miaka 27 na imepeleka wanajeshi zaidi ya 700.Kwa upande wake, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, amesema alimjulisha Katibu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, juu ya uamuzi wake huo.
Inaelezwa kuwa uamuzi huo wa kuwarejesha wanajeshi wake umelenga kuimarisha zaidi ulinzi na usalama nchini Afrika Kusini.
Hata hivyo, Rais Ramaphosa ameahidi Serikali yake kuendeleza ukaribu na mamlaka za Kinshasa katika jitihada za kurejesha hali ya usalama nchini humo.


