CAIRO, Misri
KLABU ya Al Ahly imemtoza faini kiungo wake raia wa Misri, Emam Ashour, kwa kitendo chake cha kushindwa kusafiri na kikosi kitakachoivaa Yanga.
Timu hizo zitakwaana Jumatano ya wiki ijayo, ukiwa ni mchezo wa marudiano wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ashour alijumuhishwa katika kikosi lakini hakutokea, tena bila taarifa, wakati wenzake wakisafiri kwa ndege kuja Tanzania.
Mbali ya faini, pia mchezaji huyo wa daraja la juu amefungiwa wiki mbili kuungana na kikosi hicho.
“Mkurugenzi wa Ahly, Walid Salah El-Din, ameamua kumfungia wiki mbili Emam Ashour na kumtoza faini kwa kosa la kuikosa ndege wakati wenzake wakienda Tanzania …” imeeleza taarifa ya klabu hiyo.
Hii si mara ya kwanza kwa Ashour kuadhibiwa na Al Ahly kwa vitendo vya utovu wa nidhamu. Aliadhibiwa pia Julai, 2023.
Ashour amefunga mabao 30 na kutoa ‘asisti’ 22 katika mechi 91 alizocheza tangu aliposajiliwa na Ahly msimu wa 2023-24.
Kuelekea mchezo huo wa Kundi B, Al Ahly wako kileleni mwa msimamo wakiwa na pointi saba, wakati Yanga wakiwa na nne, wakifuatiwa na FAR Rabat na JS Kabylie zenye mbili kila moja.


