CAIRO, Misri
SHIRIKISHO la Soka barani Afrika (CAF) limeziadhibu timu za taifa za Senegal na Morocco kwa vitendo vya utovu wa nidhamu vilivyooneshwa katika mechi ya fainali ya AFCON 2025 iliyochezwa Januari 18, 2026.
Mchezo huo, ambapo Senegal walishinda bao 1-0 na kutwaa ubingwa, ulisimama kwa dakika zaidi ya 10 baada ya wachezaji wa timu hiyo kugoma kuendelea kucheza.
Hatua yao hiyo ilitokana na penalti waliyopewa Morocco, ambayo hata hivyo Ibrahim Diaz alikosa hapo baadaye.
Nje ya uwanja, napo zilijitoleza ghasia nyingi, ikiwamo mashabiki wa Senegal kutifuatana na polisi waliokuwa wakijaribu kutuliza ghasia.
CAF, baada ya ukimya wa wiki zaidi ya moja, wameibuka na adhabu, ikiwamo kuyatoza faini mashirikisho ya soka ya nchi hizo, Senegal na Morocco.
Wakati huo huo, kocha wa Senegal, Pape Thiaw, ametozwa faini ya Dola 100,000 (zaidi y Sh mil. 250 za Tanzania), sambamba na kufungiwa mechi tano kwa kitendo chake cha kuwahamasisha wachezaji kutoka nje ya uwanja ili mchezo usiendelee.
Katika hatua nyingine, CA imewafungia mechi mbili kila mmoja wachezaji wa Senegal, Iliman Ndiaye na Ismaila Sarr, kwa utovu wa nidamu dhidi ya mwamuzi.
Adhabu kama hiyo imemkuta pia nahodha wa Morocco, Achraf Hakimi.
Kwa upande wake, Shirikisho la Soka la Senegal (FSF) limetozwa faini ya Dola 615,000 (zaidi ya Sh bil. 1.6), wakati Morocco wao watalipa Dola 315,000 (zaidi ya Sh mil. 806).


