MANCHESTER, Uingereza
MANCHESTER City imekamilisha usajili wa beki wa kati kutoka Crystal Palace, Marc Guehi, ambaye ametokea Crystal Palace kwa ada ya Pauni milioni 20.
Guehi alifanyiwa vipimo vya afya wikiendi iliyopita na kusaini mkataba wa miaka mitano na nusu na klabu hiyo ya jijini Manchester. Anakuwa mchezaji wa pili kutua Etihad baada ya Antoine Semenyo aliyetokea Bournemouth.
Nyota huyo aliyetokea katika ‘academy’ ya Chelsea, ameondoka Palace akiwa amecheza mechi 188 tangu ilipomsajili mwaka 2021 akitokea Swansea.
Kwa msimu huu, Guehi alishacheza mechi 20 za Ligi Kuu akiwa na kikosi cha Palace.
Man City walianza mazungumzo naye mwanzoni mwa mwezi huu baada ya kuona eneo la beki wa kati limetikiswa na majeraha ya Josko Gvardiol na Ruben Dias.
Kwa takwimu za kuanzia msimu uliopita, Guehi anaingia katika orodha ya mabeki wa kati bora kwa ‘clean sheet’, kupokonya mipira, na kucheza mipira ya juu.
Sifa nyingine kubwa aliyonayo nyota huyo wa kimataifa wa England ni uwezo wake wa kucheza nafasi nyingi katika eneo la ulinzi. Mbali ya beki wa kati, pia Guehi amekuwa akicheza pembeni (beki wa kulia na kushoto).


