Na mwandishi wetu, Gazetini
MTU wa kazi! Ndivyo unavyoweza kumwita mchezaji mpya wa Simba, Libasse Gueye, ambaye klabu hiyo imemtambulisha leo Januari 17, 2026. Nyota huyo ametua Msimbazi akitokea kwao, Senegal, alikokuwa akiitumikia Teungueth ya Ligi Kuu nchini humo.
Gueye ni mtu wa kazi kutokana na uwezo wake wa kucheza nafasi nyingi katika eneo la kiungo. Mbali ya kupiga winga zote mbili, pia anacheza eneo la kiungo mshambuliaji.
Pia, Gueye ni mtu wa kazi kutokana na kiwango bora alichokionesha katika fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) zilizofanyika mwaka 2024.
Wakati huo huo, unaweza kumwita mtu wa kazi kutokana na uchezaji wake wa kasi, pia uwezo wake mkubwa wa kutengeneza nafasi za mabao.
Gueye anaingia kwenye historia ya Simba kusajili wachezaji wanaotokea Senegal, ikikumbukwa kuwa iliwahi kuwa na Pape Ndaw na Pape Osmane Sakho.
Safari hii, mabosi wa Simba wamefunga safari hadi Senegal kumfuata Gueye ukiwa ni mkakati wa benchi la ufundi kuziba pengo la Jean Charles Ahoua.
Kama itakumbukwa, Ahoua ameondoka Simba baada ya kuiingiza klabu hiyo kiasi kizuri cha fedha kwa usajili wake wa kujiunga na vigogo wa soka la Algeria, CR Belouizdad.


