MANCHESTER, Uingereza
HATIMAYE Manchester United imetangaza kuwa kiungo wake wa zamani, Michael Carrick, ndiye atakayeinoa timu hiyo hadi mwishoni mwa msimu huu.
Je, Carrick atafanikiwa au ni kamari kama ilivyotokea kwa Ruben Amorim ambaye alitimuliwa akiwa amekalia benchi la ufundi kwa miezi 14 tu?
Enzi zake uwanjani
Carrick amerejea Man United baada ya miaka 12 ya kuitumikia timu hiyo, ambapo alicheza mechi 464 na kutwaa mataji 12, yakiwamo matano ya Ligi Kuu ya England (EPL) na moja la Ligi ya Mabingwa Ulaha.
Kwa miaka yote aliyodumu Old Trafford, hakuwahi kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi wa EPL na aliingia mara moja (2013) kwenye Kikosi Bora cha Mwaka cha Ligi Kuu hiyo.
Alipata nafasi ya kuitumikia timu ya taifa ya England mara 34. Licha ya kwenda mara tatu katika fainali za Kombe la Dunia, alicheza mechi moja pekee.
Maisha ya ukocha
Mwaka 2022, Middlesbrough ya Championship (Ligi Daraja la Kwanza England) walimpa ajira ya ukocha na aliwaahidi kuwatimizia ndoto ya kurudi EPL.
Baada ya kichapo katika mechi yake ya kwanza dhidi ya Preston, Carrick alishinda 16 kati ya 22 zilizofuata lakini mwishowe Middlesbrough ilishindwa kupanda daraja (kuingia Ligi Kuu).
Carrick alibaki klabuni hapo kwa misimu mingine miwili lakini bado hakutimiza ahadi yake ya kuiwezesha Middlesbrough kupanda Daraja.
Mabosi wa klabu hiyo waliamua kumfuta kazi. Katika utetezi wake, Carrick alisema kufeli kwake kuipandisha Daraja kulitokana na kuuzwa kwa wachezaji wake muhimu, wakiwamo Chuba Akpom aliyetimkia Ajax na Morgan Rogers aliyetua Aston Villa.
Je, ataiokoa Man United?
Carrick amewahi kuinoa Man United. Mabosi wa klabu hiyo walimpa kazi ya kusimamia timu baada ya Ole Gunnar Solskjaer kufukuzwa Novemba, 2021, na aliondoka Old Trafford baada ya ujio wa Ralf Rangnick.
Katika mechi tatu ambazo Man United ilisimamiwa na Carrick katika benchi la ufundi, timu hiyo ilishinda mbili na kutoa sare moja. Moja ya michezo aliyoshinda ni ule wa mabao 3-2 dhidi ya Washika Bunduki wa London, Arsenal.


