MADRID, Hispania
KIUNGO wa Real Madrid, Jude Bellingham, amekanusha kuwa alihusika kuushawishi uongozi wa klabu hiyo kumfuta kazi kocha Xabi Alonso.
Alonso raia wa Hispania, alifungashiwa virago muda mfupi baada ya Madrid kufungwa na Barcelona katika mchezo wa Spanish Super Cup ulizocheza higi karibuni huko Saudi Arabia.
Kwa sasa, benchi la ufundi liko chini ya mchezaji wa zamani wa vigogo hao wa La Liga na soka la Hispania kwa ujumla, Alvaro Arbeloa.
Taarifa nyingi zinadai kuwa Bellingham na Vinicius Jr walikuwa na ‘bifu’ na Alonso na walichangia uamuzi wa mabosi kumfuta kazi kocha huyo.
Akijibu madai hayo, kiungo huyo wa zamani wa Borussia Dortmund amesema: “Usiamini kila unachokisoma, ni habari zinazochochea uadui.”
Kwa upande wake, Vinicius Jr aliripotiwa kutaka kuondoka Santiago Bernabeu kwa kuwa hakuwa na uhusiano mzuri na Alonso.


