MANCHESTER, Uingereza
JINA la Oliver Glasner wa Crystal Palace linapewa kipaumbele wakati huu mabosi wa Manchester United wakiwa wanajadili kocha anayefaa kuchukua mikoba ya Ruben Amorim.
Amorim alifutwa kazi siku chache zilizopita baada ya kuliongoza benchi la ufundi kwa miezi 14 pekee tangu alipoajiriwa akitokea Sporting Lisbon ya Ureno.
Kwa mujibu wa ripoti, mabosi wa Man United wanavutiwa na kazi nzuri anayoifanya Glasner akiwa na kikosi cha Palace na huenda wakampa ajira Old Trafford.
Wakati huo huo, bado makocha wengine wenye majina makubwa katika soka la Ulaya wameendelea kuhusishwa na kibarua cha kuinoa timu hiyo.
Zipo taarifa kuwa wanaweza kumsubiri Thomas Tuchel, ambaye ataachana na timu ya taifa ya England baada ya kumalizika kwa fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu.
Ripoti zinaeleza kuwa kwa sasa uongozi wa Man United utazungumza na Ole Gunnar Solskjaer na Michael Carrick ili waliongoze benchi la ufundi hadi pale Tuchel atakapotua Old Trafford.


