Na mwandishi wetu, Gazetini
TANGU aliporejea madarakani kwa awamu yake ya pili, Rais Donald Trump amekuwa na sera zake ngumu dhidi ya mataifa ya kigeni. Kubwa zaidi ni namna alivyoivamia Venezuela na kuondoka na Rais wao, Nicolas Maduro.
Wakati hatua yake hiyo ikiendelea kukosolewa vikali, yapo mataifa mengine yaliyo hatarini kuvamiwa na Marekani na huenda ni suala la muda tu.
Greenland
Tayari Marekani ina kambi yake ya kijeshi katika Visiwa hivyo. Trump ameweka wazi kuwa wanaitaka Greenland kwa gharama yoyote.
Greenland ni Kisiwa kilichopo umbali wa maili 2,000 kutoka Kaskazini-Mashariki mwa Marekani.
Kisiwa hicho ni maarufu kwa madini yake adimu duniani, ambayo hutumika kutengeneza simu janja (smart phones), magari ya umeme na silaha za kivita.
Colombia
Saa chache tu baada ya kuishambulia Venezuela, Trump alimpa angalizo Rais wa Colombia, Gustavo Petro.
Kama alivyodai kwa Maduro, Trump amekuwa akimtaja Petro kuwa ni mfanyabiashara wa dawa za kulevya.
“Colombia inaongozwa na kiongozi anayependa kuuza cocaine,” alisema Trump alimpa angalizo raia mwenzake huyo.
Colombia, mbali ya kufahamika kwa utajiri wa mafuta na dhahabu, pia inafahamika kwa dawa za kulevya aina ya cocaine.
Iran
Iran inakabiliwa na maandamano ya raia walioingia barabarani kuipinga Serikali kutokana na hali mbaya ya kiuchumi nchini humo.
Sasa, Trump alishaionya Serikali ya Iran akisema endapo vyombo vyake vya dola vitaendelea kuua waandamanaji, basi vikosi vya Marekani vitaingilia kati.
“Tunafuatilia kwa karibuni sana. Kama wataendelea kuua raia kama ambavyo wamekuwa wakifanya, basi Marekani itawashughulikia ipasavyo,” alisema Trump.
Mwaka jana, Marekani ilishambulia vinu vya nyuklia vya Iran na hivi karibuni Trump na Benjamin Netanyahu wa Israel walikutana na kuijadili nchi hiyo kama sehemu ya mazungumzo yao.
Mexico
Kwa miaka mingi ya utawala wake, tangu awamu yake ya kwanza mwaka 2016, Trump amekuwa ‘adui’ wa Mexico.
Wakati wa kampeni za mwaka 2016, aliahidi kujenga ukuta wa kuitenganisha Marekani na Mexico. Ni ahadi iliyowatua wengi na kumpa ushawishi mkubwa.
Nini tatizo? Trump amekuwa akiilaumu Mexico kwa mambo mawili. Mosi, anasema imekuwa ikiingiza dawa za kulevya nchini mwake. Pili, ishu ya uhamiaji. Raia wa Mexico wamekuwa wakiingia Mexico.
Hivi karibuni, Trump alidai kuwa amepewa baraka zote za kuingia Mexico kukabiliana na magenge ya ‘unga’ (dawa za kulevya).
Lakini, Rais wa Mexico, Claudia Sheinbaum, amekanusha na kusema hajatoa ruhusa kwa Marekani kuingia na kuendesha operesheni yoyote katika ardhi yao.
Cuba
Marekani imekuwa adui wa Cuba yangu miaka ya 1960. Kisiwa hicho kimekuwa chini ya vikwazo vya kiuchumi vya Marekani tangu wakati huo.
Mbaya zaidi, Cuba Ina uhusiano mzuri na Maduro. Cuba na Venezuela hushirikiana kubadilishana mafuta na madaktari.
Cha kushangaza, Katibu Mkuu wa Ikulu ya Marekai, Marco Rubio, ni mtoto wa raia wa Cuba walioingia Marekani miaka mingi iliyopita.


