NEW YORK, Marekani
RAIS wa Marekani, Donald Trump, amependekeza kwa mara nyingine mpango wa kuichukua Greenland, hatua iliyozua mvutano wa kidiplomasia baada ya uongozi wa Denmark kumtaka akomeshe kile ulichoelezwa kuwa ni vitisho dhidi ya kisiwa hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari, Trump amesema Marekani “inaihitaji Greenland kwa ajili ya usalama wa taifa,” akisisitiza kuwa kisiwa hicho kina umuhimu mkubwa wa kimkakati katika masuala ya ulinzi pamoja na utajiri wa rasilimali za madini.
Trump anataka eneo hilo linalomilikiwa na Denmark lakini lenye mamlaka ya kujitawala liwe sehemu ya Marekani, hoja aliyodai inalenga kulinda maslahi ya muda mrefu ya usalama wa nchi yake, hususan katika eneo la Aktiki.
Waziri Mkuu wa Greenland, Jens Frederik Nielsen, amepinga vikali kauli hizo, akisema “inatosha sasa,” na kulielezea wazo la Marekani kutaka kudhibiti Greenland kuwa ni matamanio yasiyo na msingi.
Mvutano huo uliongezeka baada ya Waziri Mkuu wa Denmark kutoa tamko kufuatia chapisho la Katie Miller mke wa mmoja wa wasaidizi wakuu wa Trump, Stephen Miller aliyeweka kwenye mitandao ya kijamii ramani ya Greenland iliyopakwa rangi za bendera ya Marekani pamoja na neno “SOON” (HIVI KARIBUNI).
Kauli za Trump kuhusu Greenland zinakuja siku chache baada ya operesheni kubwa ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Venezuela, iliyosababisha kukamatwa kwa Rais Nicolás Maduro na mkewe, na kuhamishwa hadi New York. Hatua hiyo imeongeza hofu miongoni mwa wadau wa kimataifa kwamba Marekani huenda ikatumia nguvu za kijeshi kutafuta udhibiti wa Greenland.
Greenland, kisiwa kikubwa zaidi duniani kilichopo katika eneo la Aktiki, kina wakazi takriban 57,000 na kimekuwa kikijitawala tangu mwaka 1979, ingawa masuala ya ulinzi na sera za nje bado yanadhibitiwa na Denmark.
Licha ya ukweli kwamba wananchi wengi wa Greenland wanatamani uhuru kamili kutoka Denmark, kura za maoni zinaonesha upinzani mkubwa dhidi ya wazo la kuwa sehemu ya Marekani.



