WASHINGTON DC, Marekani
RAIS wa Marekani, Donald Trump, hababaishwi na taarifa zinazodai kuwa afya yake haiko madhubuti kwa sasa, ikichagizwa na umri mkubwa alionao.
Akiwa na miaka 79, Trump aliyerejea madarakani mwaka juzi, ndiye Rais mwenye umri mkubwa zaidi katika historia ya Marekani.
Hata hivyo, yamekuwapo madai kuwa kwa sasa kiongozi huyo hayuko sawa kiafya. Si tu kunaswa akiwa amechapa usingizi katika baadhi ya vikao, pia uwezo wake wa kusikia nao unatiliwa shaka.
Sasa, katika mahojiano yake na Jarida la The Wall Street, Rais huyo amesema alifanya vipimo vya mwili mzima miezi mitatu tu iliyopita na kubainika kuwa hana tatizo lolote.
Aidha, kupitia mahojiano hayo, Trump alionesha kusikitishwa na mjadala unaoendelea juu ya afya yake.


