15 C
New York

Trump, Zelensky watangaza maendeleo ya mazungumzo ya amani

Published:

FLORIDA, Marekani

RAIS wa Marekani Donald Trump na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky wamesema kuna maendeleo makubwa yamepatikana katika mazungumzo ya kumaliza vita vya Ukraine, ingawa suala la mpaka, hususan eneo la Donbas, bado halijapatiwa suluhu ya mwisho.

Akizungumza na waandishi wa habari katika makazi yake ya Mar-a-Lago, Florida, Zelensky alisema kuwa pande hizo mbili zimekubaliana takribani asilimia 90 ya vipengele 20 vinavyounda mpango wa amani unaojadiliwa. Kwa upande wake, Trump alisema dhamana ya usalama kwa Ukraine iko “karibu kukamilika kwa asilimia 95.”

Hata hivyo, Trump alikiri kuwa pendekezo la kugeuza eneo la Donbas mashariki mwa Ukraine-ambalo kwa kiasi kikubwa linadhibitiwa na Urusi-kuwa eneo lisilo la kijeshi bado “halijatatuliwa.”

Baadaye, Zelensky alithibitisha kuwa timu za mazungumzo za Marekani na Ukraine zitakutana wiki ijayo ili kuendeleza majadiliano, hususan kuhusu masuala nyeti yanayolenga kumaliza vita vya Urusi dhidi ya Ukraine vilivyodumu kwa karibu miaka minne.

“Tulifanya mazungumzo muhimu kuhusu masuala yote, na tunathamini maendeleo ambayo timu za Ukraine na Marekani zimepiga katika wiki zilizopita,” Zelensky alisema katika ujumbe aliouchapisha kupitia mtandao wa Telegram.

Kwa mujibu wa takwimu za sasa, Urusi inadhibiti takribani asilimia 75 ya jimbo la Donetsk na karibu asilimia 99 ya jimbo jirani la Luhansk. Mikoa hiyo miwili kwa pamoja inajulikana kama Donbas.

Moscow inaitaka Ukraine ijiondoe katika maeneo ya Donbas ambayo bado yako chini ya udhibiti wa Kyiv, wakati Ukraine ikisisitiza kuwa maeneo hayo yabaki chini ya mamlaka yake na yaweze kuanzishwa kama eneo huru la kiuchumi linalolindwa na vikosi vya Ukraine.

Urusi ilianzisha uvamizi kamili dhidi ya Ukraine mwezi Februari 2022, na kwa sasa inadhibiti takribani asilimia 20 ya eneo lote la Ukraine, kulingana na makadirio ya kimataifa.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img