DOHA, Qatar
MSHAMBULIAJI wa PSG na timu ya taifa ya Ufaransa, Ousmane Dembele, ameibuka mshindi wa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka huu wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Hii ni tuzo kubwa ya pili kwa Dembele baada ya kuibeba ile ya Ballon d’Or miezi minne iliyopita. Tuzo za FIFA zimefanyika jana Desemba 16, 2025 nchini Qatar.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 28, alistahili tuzo hiyo baada ya mafanikio yake ya msimu uliopita, ambapo aliipa PSG mataji manne, likiwamo la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Dembele aliyewahi kukipiga Barcelona na Borussia Dortmund, alisajiliwa PSG mwaka 2023 na alichangia mabao 35, yakiwamo nane ya Ligi ya Mabingwa.
Kikosi Bora FIFA
Gianluigi Donnarumma (PSG/Man City), Achraf Hakimi (PSG), Willian Pacho (PSG), Virgil van Dijk (Liverpool), Nuno Mendes (PSG), Cole Palmer (Chelsea), Jude Bellingham (Real Madrid), Vitinha (PSG), Pedri (Barcelona), Lamine Yamal (Barcelona) and Ousmane Dembele (PSG).
Tuzo ya Bao Bora
Ni maarufu kwa jina la ‘Puskas Award’ na imekwenda kwa winga wa Independiente ya Argentina, Santiago Montiel. Ni kwa bao lake la ‘tik-tak’ dhidi ya Independiente Rivadavia katika mchezo wa Ligi Kuu nchini humo.
Montiel, ambaye anakuwa Muargentina wa pili mfululizo kuitwaa tuzo hiyo baada ya Alejandro Garnacho mwaka jana, alimaliza msimu uliopita akiwa na mabao matano.
Donnarumma abeba tuzo yake
Alikuwa kipa tegemeo wa PSG wakati wa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita, wakiifunga Inter Milan katika mchezo wa fainali.
Wakati huo huo, alimaliza msimu uliopita akiwa ameipa timu hiyo mataji mengine matau, likiwamo la Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1).
Hiyo imemfanya Muitalia huyo anayeitumikia Manchester City kwa sasa kutwaa tuzo ya Kipa Bora wa Mwaka huu wa FIFA.
Donnarumma ameitwaa tuzo hiyo akiwapiku walinda mlango wengine watatu; Alisson Becker, Emi Martinez, David Raya na Thibaut Courtois.
Enrique amfunika Slot
Akiwa ndiye kocha wakati PSG ilibeba mataji manne msimu uliopita, Luis Enrique amestahili kuwa Kocha Bora wa Mwaka huu wa FIFA.
Enrique (55), aliajiriwa na matajiri hao wa Paris tangu mwaka 2023 na ubingwa wake wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita ulikuja akiwa amezifunga timu kubwa, zikiwamo Liverpool, Arsenal na Inter Milan.
Ameichukua tuzo hiyo ya Kocha Bora wa FIFA akiwafunika kocha wa Liverpool, Arne Slot, na Hansi Flick wa Barcelona.


