WASHINGTON DC, Marekani
MAKAMU Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani (FBI), Dan Bongino, amesema atajiuzulu wadhifa huo ifikapo Januari, mwakani.
Katika taarifa yake aliyochapisha katika ukurasa wa X (zamani Twitter), Bongino amewashukuru Rais Trump, Mkurugenzi wa FBI na Mwanasheria Mkuu kwa nafasi aliyokuwa nayo.
Ni chini ya mwaka mmoja tu tangu alipoteuliwa na Rais Trump na hivi karibuni alisifiwa na ‘bosi’ wake huyo kwa kazi nzuri aliyoifanya.
“Nitaiacha nafasi yangu hii ndani ya FBI ifikapo Januari. Nataka kuwashukuru Rais Trump, Mwanasheria Mkuu (Pam Bondi), na Mkurugenzi (Kash Patel) kwa fursa hii ya kuhudumu kimkakati,” ameandika.
Bongino, ambaye aliteuliwa Februari, mwaka huu, amewahi kuwa Ofisa wa polisi wa New York na aliwahi pia alikuwa sehemu ya ulinzi wa Rais Barack Obama.
“Muhimu zaidi, niwashukuru ninyi Wamarekani wenzangu kwa heshima ya kuwahuhudumia. Mungu ibariki Marekani na wote wanaoilinda,” amesisitiza Bongino.
Ikumbukwe, uteuzi wake kuwa Makamu Mkurugenzi wa FBI ulikosolewa hata na taasisi hiyo ya usalama yenye waajiriwa takribani 14,000.


