18 C
New York

Takwimu zinazomkaba kocha Spurs

Published:

LONDON, Uingereza

MATOKEO ya kufungwa mabao 3-0 na Nottingham Forest katika mchezo uliopita yameifanya Tottenham kushika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England (EPL).

Kwa maana, Spurs inabaki ikihitaji pointi sita ili kuifikia ‘Top Four’, mwenendo ambao unampa presha kubwa kocha wa timu hiyo, Thomas Frank.

Takwimu zinaonesha kuwa Frank amepoteza mara nyingi kuliko mechi alizoshinda, pia akifungwa tatu kati ya tano za hivi karibuni.

Kama hiyo haitoshi, dhidi ya Forest ilikuwa ni mechi ya 25 kwa Frank kuiongoza Tottenham tangu alipoajiriwa akitokea Brentford.

Katika michezo hiyo, kocha huyo wa kimataifa wa Denmark ameshinda 10 na kufungwa tisa. Mechi tisa alizopoteza ni pamoja na ile ya kichapo cha penalti kutoka kwa PSG katika mchezo wa UEFA Super Cup.

Pia, ni pamoja na kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Newcastle United katika mchezo wa Kombe la Ligi (Carabao Cup).

Wakati huo huo, pia kuna mchezo waliofungwa mabao 4-1 na majirani zao, Arsenal, katika ‘derby’ ya Kaskazini mwa Jiji la London.

Ni kutokana na mwenendo huo usioridhisha, mashabiki wa Tottenham wameanza kumkumbuka kocha Ange Postecoglou.

Postecoglou raia wa Australia, alifukuzwa na nafasi yake kuchukuliwa na Frank ambaye aliwavutia mabosi wa Tottenham kutokana na kazi nzuri aliyoifanya akiwa na Brentford.

Tofauti na Frank ambaye ameshinda mechi 10 kati ya 25, Postecoglou alipata ushindi mara 14 katika idadi hiyo ya michezo yake ya kwanza klabuni hapo.

Kubwa zaidi, kocha huyo aliiwezesha Tottenham kutwaa Ligi ya Europa, taji la kwanza klabuni hapo baada ya ukame wa miaka 17.

Hata hivyo, mashabiki wa Tottenham hawapaswi kusahau kilichotokea katika mechi 25 za mwishoni mwa msimu uliopita chini ya kocha huyo mwenye umri wa miaka 60.

Alifungwa 13 na kushinda tisa pekee na timu hiyo ikamaliza msimu ikiwa nafasi ya 17 kwenye msimamo. Ni nafasi mbaya zaidi katika historia yao Ligi Kuu.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img