KYIV, Ukraine
WAKAZI zaidi ya milioni moja wanakosa huduma ya umeme nchini Ukraine na hiyo imesababishwa na mashambulizi makali ya Urusi kwa majirani zao hao.
Urusi imeendelea kulishambulia Ukraine, licha ya jitihada zilizopo za Rais Donald Trump katika kumaliza vita ya nchi hizo za Mashariki mwa Ulaya.

Ifahamike kuwa ujumbe maalumu wa Marekani ukiongozwa na Steve Witkoff na Jared Kushner wanatarajiwa kukutana na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, na viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Berlin.
Ikulu ya Marekani mjini Washington imekuwa ikisisitiza kuwa Rais Trump anahuzunishwa na mgogoro uliopo kati ya Ukraine na Urusi.
Sasa, wakati jitihada hizo za kumaliza vita zikiendelea, Rais Zelenskyy amethibitisha kuwa Urusi imefanya mashambulizi ya anga zaidi ya 450 usiku wa jana Desemba 12, 2025.
Rais Zelenskyy amesema Mji wa Odesa, ambao uko Kusini mwa Ukraine, ndiyo ulioathirika zaidi na changamoto ya kukosa huduma ya umeme.


