LAGOS, Nigeria
WAKATI huu kukiwa na mfululizo wa matukio ya utekaji yanayofanywa na vikundi vya waasi nchini Nigeria, Waziri wa Ulinzi ametangaza kujiuzulu. Hata hivyo, kwa mujibu wa kile kilichoelezwa na Serikali, Mohammed Badaru Abubakar amejiuzulu kutokana na sababu za kiafya.
Nigeria imekuwa kwenye hali mbaya ya usalama, hasa kwa wiki za hivi karibuni, ambapo yamekuwapo matukio mengi ya waasi kuvamia na kuteka wananchi.
Katika tukio la hivi karibuni, waasi wakiwa na silaha, zikiwamo bunduki, walivamia kanisa wakati wa Ibada ya Jumapili na kuondoka na mchungaji, pamoja na waumini zaidi ya 10. Kabla ya hilo, tukio jingine lililotikisa ni lile la mjini Sakoko, ambapo waasi kuvamia sherehe na kuteka watu 30, akiwamo bi harusi.
Lakini, kubwa zaidi ni lile la waasi kuvamia Shule ya St. Mary mjini Papiri na kuteka watu 315, wengi wao wakiwa ni wanafunzi. Ni kwa kipindi kifupi tu cha wiki mbili zilizopita, waasi wameteka watu takribani 490 katika maeneo mbalimbali, kwa mujibu wa Gazeti la Punch la Nigeria.


