LONDON, Uingereza
KLABU ya Arsenal imeripotiwa kupiga hatua kubwa katika harakati zake za kuinasa saini ya mshambuliaji wa Real Madrid na timu ya taifa ya Brazil, Vinicius Jr.
Nyota huyo anataka kuondoka Madrid, huku mambo mawili yakitajwa kuwa sababu ya kupoteza mapenzi yake kwa klabu ya Madrid.
Mosi, Vinicius ameripotiwa kukorofishana na kocha wa kikosi hicho, Xabi Alonso, ikifikia hatua ya wawili hao kurushiana maneno katika moja ya michezo yao msimu huu.
Pili, mshambuliaji huyo anaiona thamani yake ikiwa imeshuka tangu klabu hiyo ilipomsajili staa wa timu ya taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappe.
Kwa mujibu wa ripoti, Arsenal wanafuatilia kila hatua ya mazungumzo ya mkataba mpya kati ya Vinicius na Madrid, ambapo staa huyo anataka alipwe mshahara kama anaopewa Mbappe.
Taarifa zinaeleza pia, ‘Washika Bunduki’ wa London wako tayari kuvunja rekodi yao ya usajili kwa kutumia Pauni milioni 132 kumchukua Mbrazil huyo.
Vinicius, ambaye alijiunga na Madrid akitokea Flamengo ya Ligi Kuu nchini Brazil, amefunga mabao matano na kutoa ‘asisti’ nne katika dakika 1,172 alizocheza.
Published:


