12.6 C
New York

Ronaldo ndani mechi ya kwanza Kombe la Dunia

Published:

LISBON, Ureno
LICHA ya kadi nyekundu, nahodha wa timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo, hatakosa mechi ya kwanza ya fainali zijazo za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani huko Marekani, Canada na Mexico.
Awali, ilikuwepo hofu kuwa angekosa mechi tatu, ikiwamo ya kwanza ya fainali hizo, kutokana na kadi nyekundu aliyolimwa katika mechi ya kufuzu dhidi ya Ireland.
Kama itakumbukwa, mshambuliaji huyo wa Al Nassr ya Saudi Arabia alipewa kadi nyekundu hiyo baada ya kumpiga kiwiko beki wa Ireland, Dara O’Shea.
‘CR 7’ ameshatumikia adhabu ya kukosa mechi moja, ambapo hakuwa uwanjani wakati Ureno ikimenyana na Armenia katika mchezo wa mwisho wa kufuzu Kombe la Dunia.
Sasa, zikiwa zimebaki mechi mbili, Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) imeamua kuwa adhabu hiyo itasogezwa mbele kwa mwaka mmoja.
Kwa upande wake, kocha wa timu ya taifa ya Ureno, Roberto Martinez, alimkingia kifua Ronaldo baada ya kadi nyekundu aliyopewa katika mchezo wao na Ireland akisema:
“Kadi nyekundu aliyopewa nahodha ni ya kwanza katika michezo 226. Nafikiri anastahili pongezi. Nafikiri alifanya vibaya lakini ni kwa ajili ya kuipambania timu.”
Mwanzoni mwa mwaka huu, Ronaldo mwenye umri wa miaka 40 aliweka wazi kuwa fainali zijazo zitakuwa za mwisho kwake kucheza Kombe la Dunia.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img