23.2 C
New York

Arsenal haishikiki EPL, ‘ukuta’ waipa jeuri

Published:

LONDON, Uingereza
BAADA ya mechi za wikiendi iliyopita, sasa Arsenal wako kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya England (EPL) wakiwa wameizidi pointi nne timu inayoshika nafasi ya pili, Bournemouth.
Arsenal wakiwa na pointi zao 22 dhidi ya 18 za Bournemouth, wako kwenye nafasi hiyo huku kila timu ikiwa imeshacheza mechi tisa msimu huu.
Kufikia hatua hii, Arsenal ndiyo timu pekee iliyoshinda mechi nyingi (7), ikifungwa moja na kupata sare moja.
Kwa upande mwingine, siri kubwa ya ubora wa ‘Washika Bunduki’ ni safu yao ya ulinzi inayoongozwa na Gabriel na William Saliba.
Safu yao hiyo imeifanya Arsenal kuwa timu pekee iliyoruhusu mabao machache (3) kufikia hatua hii ya msimu wa Ligi Kuu hiyo ya EPL.
Timu zinazofuata kwa kufungwa mabao machache ni Tottenham, Sunderland na Manchester City, ambazo hata hivyo kila moja imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara saba.
Katika mechi tisa, Arsenal imecheza sita bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa (clean sheets), pia ikiwa imeruhusu mashuti 19 pekee kulenga lango lake.
Dhidi ya Crystal Palace katika mchezo uliopita, ambao Arsenal wakiwa Emirates walishinda bao 1-0, wapinzani wao walipiga shuti moja pekee lililolenga lango kwa dakika zote 90.
“Kwa namna Arsenal inavyocheza, inaweza kupata matokeo mbele ya timu yoyote. Timu inayotaka ubingwa huwa hairuhusu mabao mengi, ndicho wanachokifanya,” amesema winga wa zamani wa Arsenal, Theo Walcott.
Kwa upande mwingine, Arsenal chini ya kocha Mikel Arteta wamekuwa wakinufaika kwa kiasi kikubwa na mipira ya kutenga (faulo na kona).
Mathalan, walitumia njia hiyo kupata mabao katika mechi muhimu dhidi ya Manchester United, Newcastle, Fulham na Atletico Madrid waliyocheza nayo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kati ya mabao yao 16 waliyofunga msimu huu wa EPL, 11 (69%) yalitokana na staili hiyo ya mipira ya kutenga.
Kwamba wakali hao wa Kaskazini mwa London ndiyo timu tishio zaidi kwa mabao ya aina hiyo, wakifuatiwa na majirani zao, Chelsea (9).

Related articles

Recent articles