23.5 C
New York

Zimbabwe yatimua kocha kisa Kombe la Dunia

Published:

HARARE, Zimbabwe
MATOKEO mabaya katika mechi za kufuzu fainali zijazo za Kombe la Dunia yamesababisha kocha wa timu ya taifa ya Zimbabwe ‘Warriors’, Michael Nees, afungashiwe virago.
Chama cha Soka cha Zimbabwe (ZIFA) kimetangaza uamuzi huo leo, hivyo kuhitimisha kibarua cha Mjerumani huyo aliyeajiriwa Septemba, mwaka jana.
Katika mechi 16 alizokaa kwenye benchi la ufundi, Warriors imeshinda mbili pekee na zote ni dhidi ya Namibia mwaka jana.
Zimbabwe ilimaliza mkiani mwa Kundi C katika mechi za kuwania tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia za mwakani.
Kwa mujibu wa msimamo, Zimbabwe ilijikuta mkiani baada ya kukosa ushindi katika mechi zote 10, ikifungwa tano na kutoa sare tano.
“Chama cha Soka kinatumia nafasi hii kumshukuru Nees kwa jitihada zake na mchango wake katika soka la Zimbabwe,” imeeleza taarifa ya ZIFA.
Wakati huo huo, ZIFA imeweka wazi kuwa tayari imeingia mawindoni kusaka kocha mpya atakayekiongoza kikosi katika michuano ya AFCON.

Related articles

Recent articles