MADRID, Hispania
MECHI za Ligi Kuu ya La Liga zimeendelea kushuhudia wachezaji wakisimama bila kucheza mpira kwa sekunde 15 za mwanzo.
Kitendo hicho kinatumika kama ujumbe wa wachezaji kutokukubaliana na uamuzi wa Bodi ya La Liga kuamua baadhi ya mechi zichezwe Marekani.
Wikiendi iliyopita, matukio ya aina hiyo yalijitokeza katika mechi zilizozihusisha Barcelona na Atletico Madrid, ambazo zilikuwa zikivaana na Girona na Osasuna.
Awali, wachezaji wa Oviedo na Espanyol walifanya hivyo wakati timu hizo zilipovaana Ijumaa.
Ni kama ilivyokuwa katika mechi zingine mbili; Sevilla dhidi ya Mallorca na Villarreal iliyocheza na Real Betis.
Agosti, mwaka huu, Shirikisho la Soka la Hispania (RFEF) lilipitisha uamuzi wa mechi kati ya Villarreal na Barcelona kuchezwa Marekani ifikapo Desemba 20.
Uamuzi huo ulipingwa na Chama cha Wanasoka (AFE) na kutangaza kuwa kimekubaliana na manahodha wa timu zote za La Liga kugomea mpango huo.
Published:


