11.6 C
New York

Mastaa hawa hawauziki soko la usajili Ulaya

Published:

LONDON, Uingereza
NI takribani wiki mbili tu zimebaki kabla ya kufungwa kwa dirisha kubwa la usajili la majira haya ya kiangazi.
Hata hivyo, kwa baadhi ya wachezaji wenye majina makubwa, wamejikuta kwenye wakati mgumu wa kupata klabu za kujiunga nazo.
Mbaya zaidi, hawaonekani kuhitajika katika klabu walizopo sasa. Je, ni akina ani hao? Makala haya yanachambua.
Gianluigi Donnarumma (PSG)
Tangu alipokorofishana na kocha
Luis Enrique, kipa huyo ameonekana kupoteza nafasi kwenye mipango ya Mhispania huyo.
Donnarumma, raia wa Italia aliyewahi kuitumikia AC Milan, anahusishwa na Manchester United, Manchester City na Chelsea lakini hakuna ofa iliyofika mezani.
Tyrell Malacia (Man United)
Msimu uliopita, Malacia alipelekwa kwa mkopo PSV Eindhoven ya Uholanzi. Mlinzi wa kushoto huyo hahitajiki Old Trafford.
Kwa misimu mitatu aliyodumu Manchester United, nyota huyo anayecheza pia eneo la beki wa kulia, amecheza mechi 16 tu za Ligi Kuu akiwa kikosi cha kwanza.
Ben Chilwell (Chelsea)
Beki wa kushoto huyo hajacheza mechi yoyote ya Chelsea kwenye Ligi tangu Aprili, mwaka jana.
Msimu uliopita, alikuwa Crystal Palace kwa mkopo. Blues wanasaka klabu inayomtaka nyota huyo mwenye umri wa miaka 28.
Jakub Kiwior (Arsenal)
Arsenal walitumia kitita cha Pauni milioni 17 kumsajili akitokea Spezia ya Italia mwaka 2023.
Hata hivyo, licha ya kufanya vizuri pindi alipoziba pengo la Gabriel, bado nyota huyo raia wa Poland hana nafasi Emirates kutokana na uwepo wa William Saliba na beki mpya, Cristhian Mosquera.
Oleksandr Zinchenko (Arsenal)
Zinchenko amecheza jumla ya mechi 145 za Ligi Kuu akiwa na timu mbili tofauti; Manchester City na Arsenal.
Zinchenko amepoteza nafasi ya kuanza, kiasi kwamba hata beki wa kulia, Jurrien Timber, amekuwa akitumika kwenye eneo lake.
Kalvin Phillips (Manchester City)
Kiungo huyo hajaitumikia Manchester City katika mechi za Ligi tangu Novemba, 2023. Amecheza mechi 16 tu za Ligi tangu mwaka 2022.
Hivi karibuni, aliishia kucheza kwa mkopo katika klabu za West Ham na Ipswich Town.
Yves Bissouma (Tottenham)
Tottenham alitumia Pauni milioni 25 kumsajili Bissouma akitokea Brighton mwaka 2022.
Licha ya kushuka kiwango, hivi karibuni alimchefua kocha mpya, Thomas Frank, kutokana na tabia yake ya kuchelewa mazoezini.
Raheem Sterling (Chelsea)
Sterling amebakiza miaka miwili katika mkataba wake na Blues, ambapo analipwa Pauni 300,000 kwa wiki pale Stamford Bridge.
Hana nafasi klabuni hapo baada ya kurejea akitokea Arsenal alikokuwa kwa mkopo msimu uliopita.
Nicolas Jackson (Chelsea)
Alisajiliwa mwaka 2023 na kupewa mkataba wa miaka nane. Msimu uliopita, mshambuliaji huyo alifunga mabao 10 kwenye mechi za Ligi Kuu.
Kocha mpya, Enzo Maresca, haonekani kumuhitaji Jackson, licha ya kwamba Msenegal huyo amekuwa straika tegemeo kwa Blues.
Christopher Nkunku (Chelsea)
Nkunku alimaliza msimu uliopita akiwa amefunga mabao matatu pekee ya Ligi Kuu, likiwamo la ushindi katika mchezo dhidi ya Bournemouth.
Sasa, ujio wa Liam Delap na Joao Pedro unaashiria kuwa Mfaransa huyo hana nafasi kikosini.
Alejandro Garnacho (Man United)
Tangu alipojiunga na Manchester United, Garnacho raia wa Argentina amefunga mabao 16 kwenye mechi za Ligi Kuu.
Garnacho mwenye umri wa miaka 21, haonekani kuwa kwenye mipango ya msimu huu ya kocha Ruben Amorim.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img