MUNICH, Ujerumani
USAJILI wa majira haya ya kiangazi umeshuhudia baadhi ya wachezaji wenye majina makubwa wakiipa kisogo Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga).
Florian Wirtz aliondoka Bayern Leverkusen na kujiunga na Liverpool ya England. Nyota huyo wa kimataifa wa Ujerumani alitimkia Anfield, licha ya kutakiwa na vigogo wa Bundesliga, Bayern Munich.
Kwa upande mwingine, mkongwe wa Bayern Munich, Thomas Muller, alichagua kwenda Ligi Kuu ya Marekani (MLS), akiondoka Bayern na kujiunga na Vancouver Whitecaps.
Pia, kiungo wa pembeni wa Bayern, Kingsley Coman, ambaye alifunga bao la ushindi wakati Bayern ilipotwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2020, alijiunga na Al-Nassr ya Saudi Arabia.
Wakati Ligi Kuu hiyo ya Ujerumani ikipoteza mastaa hao, mchezaji pekee mwenye jina kubwa aliyetua ni Luis Diaz aliyejiunga na Bayern akitokea Liverpool.
Kama ilivyokuwa kwa Wirtz, Bayern ilijaribu kumsajili Nico Williams lakini winga huyo alichagua kuongeza mkataba katika klabu yake ya Athletic Bilbao.
Licha ya kufeli huko, Mkurugenzi wa Michezo wa Bayern, Max Eberl, anasikika akijibu madai ya klabu hiyo kupoteza mvuto mbele ya wachezaji wenye majina makubwa.
“Anayesema Bayern haiwavutii tena wachezaji wakubwa halijui soko. Bayern ina uwezo wa kumsajili mchezaji yeyote inayemtaka,” anasema.
Hata hivyo, kauli yake inapingana na maoni ya Mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo, Oliver Kahn, anayesema Bundesliga imepoteza mvuto wake kwa mastaa wakubwa wa soka.
“Kitendo cha Florian Wirtz kuikataa Bayern kwa ajili ya Liverpool kinapaswa kutufikirisha. Ligi Kuu ya England imejiweka kwenye kiwango cha kumfanya kila mchezaji aamini kuwa anaihitaji ili kufika mbali zaidi,” anasema kipa huyo wa zamani wa Bayern na timu ya taifa ya Ujerumani.
Ukiweka kando maoni ya Khan, takwimu zinampinga Erbel zikionesha kuwa Bundesliga imeporomoka katika ushindani wa soka la Ulaya. Hakuna taji kubwa (Ligi ya Mabingwa, Ligi ya Europa au Kombe la Dunia kwa ngazi ya Klabu) lililotua katika ardhi ya Ujerumani tangu mwaka 2022.
Mara ya mwisho kwa timu kubwa zaidi, Bayern, kuwa mabingwa wa Ligi ya Mabingwa ni mwaka 2020. Miaka miwili baadaye, Eintracht Frankfurt wakatwaa taji la Ligi ya Europa.
Aidha, hata viwango vya ubora wa soka vya Shirikisho la Soka barani Ulaya (UEFA) vinathibitisha anguko la Bundesliga. Ligi hiyo inashika nafasi ya nne, nyuma ya EPL, Serie A na La Liga.
Kwa upande uchumi, licha ya kuvuna mapato ya euro bilioni 4.8 kwa msimu wa 2023-24, bado Bundesliga inashika nafasi ya pili barani Ulaya, ikizidiwa na EPL inayoongoza kwa euro bilioni 7.4.
Kwa msimu huu wa 2025-26, EPL itavuna euro bilioni 1.95 kutokana na mapato ya haki za matangazo ya televisheni, wakati Bundesliga itaambulia euro bilioni 1.12.
Mwisho, hata idadi ya mashabiki wanaoingia uwanjani kutazama mechi za Bundesliga imeporomoka kwa kasi nchini Ujerumani. Msimu uliopita, EPL ilikuwa na mashabiki 40,474, wakati mechi za Bundesliga ziliingiza mashabiki 38,662.
Published:


