9.3 C
New York

United, Arsenal moto utawaka wikiendi hii

Published:

LONDON, England
MECHI kubwa ya kwanza msimu huu wa Ligi Kuu ya England (EPL), ambapo Jumapili hii Manchester United watakuwa nyumbani Old Trafford kuwakaribisha Washika Bunduki wa London, Arsenal.
Kwa upande mwingine, straika mpya wa Arsenal, Viktor Gyokeres, atakutana kwa mara ya kwanza na kocha aliyekuwa naye Sporting Lisbon, Ruben Amorim, ambaye kwa sasa anainoa Man United.
MAN UNITED
Vijana wa kocha Amorim wamemaliza ‘pre-season’ yao bila kupoteza. Walishinda mechi mbili dhidi West Ham United na Bournemouth, kisha sare (Leeds United na Everton), kabla ya ushindi mwingine mbele ya Fiorentina.
Dhidi ya Arsenal kesho, Andre Onana atasimama langoni. Katika eneo la beki wa kati, kocha Amorim ataanza na wawili kati ya Leny Yoro, Matthijs de Ligt au Harry Maguire.
Mmoja wao atacheza kulia huku Luke Shaw au kinda Ayden Heaven akitokea kushoto kuziba pengo la Lisandro Martinez anayeuguza majeraha.
Kwa mara ya kwanza, Benjamin Sesko atacheza mechi ya ushindani akiwa na Man United, akitarajiwa kuiongoza safu ya ushambuliaji.
Nyuma yake, kwa maana ya kiungo mshambuliaji (namba 10), atakuwepo staa mwingine mpya kikosini, Matheus Cunha.
Eneo la kiungo wa kati litaendelea kuwa chini ya ‘fundi’ wa Kireno, Bruno Fernandes, akisaidiwa majukumu ya kukaba na Manuel Ugarte au Casemiro. Kobbie Mainoo anaweza kutumika pia katika eneo hilo.
ARSENAL
Washika Bunduki walianza ‘pre-season’ yao barani Asia kwa ushindi dhidi ya AC Milan na Newcastle United, kabla ya kufungwa na wapinzani wao wa London, Tottenham.
Waliporejea nyumbani, England, Arsenal walipoteza mbele ya Villarreal, kisha kupata ushindi dhidi ya vigogo wa La Liga, Athletic Bilbao.
Ni wazi kocha Mikel Arteta ataanza na David Raya langoni, akisaidiwa na mabeki wa kati, William Saliba na Gabriel, wakati Riccardo Calafiori na Myles Lewis-Skelly wakicheza pembeni (kulia na kushoto).
Kwa upande wa eneo la kiungo, matarajio ni kuwaona Martin Zubimendi, Declan Rice na Martin Odegaard.
Ukija upande wa winga ya kulia, ni wazi kocha huyo atachagua kuanza na Bukayo Saka, huku staa wa Kibrazil, Gabriel Martinelli, akitokea kushoto.
Katika eneo la ushambuliaji, Arteta ataanza na Kai Havertz au Gyokeres, ingawa pia anaweza kuwatumia wote katika eneo la ushambuliaji ili kuwapata wakati mgumu mabeki wa Old Trafford.
REKODI HIZI HAPA
Man United haijafungwa na Arsenal katika mechi mbili zilizopita. Mara ya mwisho kwa timu hizo kukutana ni Mei, mwaka huu, ambapo Man United ilishinda kwa penalti katika mechi ya FA.
Hata hivyo, kabla ya michezo miwili hiyo, Arsenal ilikuwa na rekodi nzuri ya kushinda mara nne mfululizo mbele ya Mashetani Wekundu hao wa Old Trafford.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img