8.4 C
New York

Nyota hawa watashangaza wengi msimu huu EPL

Published:

LONDON, England
MSIMU mpya wa uhondo wa mechi za Ligi Kuu ya England (EPL) ulianza jana. Kama ilivyo kawaida, wapo wachezaji wanaopewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri msimu huu wa 2025-26.
Hata hivyo, kuna wachezaji wanaochukuliwa poa lakini huenda msimu ukamalizika majina yao yakiwa makubwa. Ni akina nani hao? Makala haya yanachambua.
ESTEVAO WILLIAN (CHELSEA)
Akiwa na umri wa miaka 18, winga huyo raia wa Brazil ameanza kuitwa ‘Messi mdogo’ kutokana na uwezo wake mkubwa ndani ya uwanja.
Chelsea walitumia Pauni milioni 29 kumng’oa Palmeiras ya Ligi Kuu ya Brazil.
Estevao alifunga bao katika mechi yake ya kwanza (dhidi ya Bayern Leveskusen).
JOEL PIROE (LEEDS UNITED)
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uholanzi ana umri wa miaka 26. Piroe ndiye mfungaji bora wa Championship msimu uliopita baada ya kuingia kambani mara 19.
Ikumbukwe, mchango wake huo wa mabao uliiwezesha Leeds United kutwaa ubingwa na kukata tiketi ya kurejea Ligi Kuu ya England.
CRISTHIAN MOSQUERA (ARSENAL)
Beki wa kati huyo raia wa Hispania ana umri wa miaka 21. Ni mzuri katika matumizi ya miguu yote.
Msimu uliopita, Mosquera alikuwa Valencia, ambapo alikosa mechi tatu pekee. Arsenal wamemnasa kwa Pauni milioni 13 tu.
DAN NDOYE (NOTTINGHAM FOREST)
Mshambuliaji wa kimataifa wa Uswis, ambaye ana umri wa miaka 24. Amekuwa pia akitumika katika eneo la kiungo wa pembeni.
Ndoye mwenye asili ya Senegal anakotokea baba yake, alianza kupata jina akiwa FC Basel, kabla ya kuwika pia alipokuwa Bologna.
EL HADJI MALICK DIOUF (WEST HAM UNITED)
Huyo ni mlinzi wa kushoto, ambaye pia ni winga. Diouf ana umri wa miaka 20 na ni raia wa Senegal. Ametua West Ham kwa Pauni milioni 19 akitokea Slavia Prague.
Akiwa mdogo, Diouf alikuwa shabiki wa beki wa Kibrazil aliyewahi kuwika barani Ulaya akiwa na Real Madrid. Amekuwa akivaa jezi namba 12 kwa kipindi chote cha maisha yake ya soka.
EMMANUEL AGBADOU (WOLVES)
Mlinzi wa kati wa Wolves, raia wa Ivory Coast mwenye umri wa miaka 28. Ametua EPL akitokea Ligue 1, ambako alikuwa nahodha wa Reims.
Agbadou mwenye urefu wa futi 6 na inchi 4, ni mchezaji wa kwanza kusajiliwa na kocha mpya wa Wolves, Vitor Pereira, dili hilo likigharimu kitita cha Pauni milioni 17.
JUSTIN DEVENNY (CRYSTAL PALACE)
Kiungo wa kimataifa wa Jamhuri ya Ireland ya Kaskazini. Nyota huyo ana umri wa miaka 21. Ndiye aliyepiga penalti ya ushindi iliyoipa Palace taji la Ngao ya Jamii katika mchezo dhidi ya Liverpool.
Devenny alizaliwa Scotland lakini alichagua kuiwakilisha Ireland anakotokea mama yake. Ameshacheza mechi tano akiwa na jezi za Taifa hilo.
SIMON ADINGRA (SUNDERLAND)
Ni winga raia wa Ivory Coast na umri wake ni miaka 23. Adingra alikuwa sehemu ya kikosi kilichobeba ubingwa wa AFCON mwaka 2023, akitoa ‘asisti’ zote katika ushindi wa mabao 2-1 wa mechi ya fainali dhidi ya Nigeria.
Adingra ndiye aliyekuwa Kinda Bora wa mashindano hayo ya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF). Sunderland wamelipa Pauni milioni 18 kumng’oa Brighton.
JHON ARIAS (WOLVES)
Nyota huyo raia wa Colombia ni winga, ingawa pia amekuwa akitumika katika eneo la kiungo – mshambuliaji (namba 10). Arias ana umri wa miaka 27.
‘Pele wa Colombia’ amejiunga na Wolves akitokea Fluminense ya Ligi Kuu nchini Brazil. Alitwaa mara tatu tuzo ya nyota wa mchezo katika michuano ya Kombe la Dunia kwa ngazi ya Klabu iliyomalizika hivi karibuni huko Marekani.
DIEGO COPPOLA (BRIGHTON)
Umri ni miaka 21 na ni beki wa kati raia wa Italia. Brighton imemng’oa Serie A alikokuwa akiitumikia Hellas Verona. Urefu wake ni futi 6 na inchi 4.
Coppola alianzia soka lake katika ‘academy’ ya klabu hiyo na msimu uliopita alikosa mechi nne pekee za Ligi Kuu hiyo ya Italia.
ROMAIN ESSE (CRYSTAL PALACE)
Kiungo wa kimataifa wa England. Esse ana umri wa miaka 20. Januari, mwaka huu, alitua Palace akitokea Millwall aliyojiunga nayo akiwa na miaka tisa, baada ya kufeli majaribio pale Chelsea.
Changamoto kubwa aliyonayo ni kupata nafasi ya kuanza mbele ya Eberechi Eze na Ismaila Sarr wanaounda ‘pacha’ ya safu ya ushambuliaji ya Palace.
HARRY HOWELL (BRIGHTON)
Msimu uliopita, kiungo huyo raia wa England aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa Brighton mwenye umri mdogo zaidi kucheza EPL. Howell ana miaka 17.
Aliandika historia hiyo alipoingia akitokea benchi na kuiwezesha Brighton kupata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya ‘Majogoo’ wa Anfield, Liverpool.
JAIR CUNHA (NOTTINGHAM FOREST)
Beki wa kati raia wa Brazil. Cunha ana umri wa miaka 20. Alisajiliwa Juni, mwaka huu, akiwa mchezaji wa pili kusajiliwa na Forest akitokea Botafogo ya Brazil baada ya Igor Jesus.
Cunha, ambaye pia ni mtaalamu wa mabao ya vichwa, alikuwa mchezaji muhimu kwa U-20 ya Brazil iliyotwaa ubingwa wa michuano ya mwaka huu ya Amerika ya Kusini.
MAXI DOWMAN (ARSENAL)
Umri ni miaka 15 tu lakini tayari kiungo huyo wa kimataifa wa England ameanza kuyavutia macho ya mawakala wengi wa soka barani Ulaya.
Dowman alianza kufanya mazoezi na timu ya wakubwa ya Arsenal akiwa na umri wa miaka 14 tu. Kocha Mikel Arteta alimtumia kuchukua nafasi ya Bukayo Saka katika mechi mbili za ‘pre-season’.
HABIB DIARRA (SUNDERLAND)
Kiungo huyo raia wa Senegal ana umri wa miaka 21 ameigharimu Sunderland kitita cha Pauni milioni 30 akitokea Ufaransa alikokuwa akiitumikia klabu ya Strasbourg.
Diarra alikuwa nahodha wa kikosi cha Strasbourg kilichomaliza msimu uliopita kikiwa na tiketi ya kushiriki michuano ya Ulaya.
RIO NGUMOHA (LIVERPOOL)
Winga raia wa England mwenye umri wa miaka 16. Alifunga mabao mawili katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Athletic Bilbao.
Januari, mwaka huu, nyota huyo aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kucheza kikosi cha kwanza cha Liverpool kwenye michuano ya Kombe la FA.
THIERNO BARRY (EVERTON)
Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 22 anacheza eneo la ushambuliaji. Msimu uliopita, alikuwa Villarreal na kufunga mabao 11 na ‘asisti’ nne katika mechi 38.
Mchango wake kikosini uliiwezesha timu hiyo kumaliza msimu ikiwa nafasi ya tano kwenye msimamo wa La Liga. Everton wamemsajili kwa Pauni milioni 27.
JOSH KING (FULHAM)
Akiwa na umri wa miaka 18 kwa sasa, King anayecheza eneo la kiungo alianzia soka lake katika ‘academy’ ya Fulham. Alicheza U-9 ya klabu hiyo.
Je, ‘dogo’ huyo atafanikiwa kuanzia kikosini mbele ya wazoefu Andreas Pereira na Emile Smith Rowe aliyesajiliwa kwa ada iliyovunja rekodi ya usajili klabuni hapo?
JAKA BIJOL (LEEDS UNITED)
Raia huyo wa Slovenia mwenye umri wa miaka 26 anacheza eneo la beki wa kati. Leeds walimsajili Juni, mwaka huu, kwa Pauni milioni 15 akitokea Udinese.
Bijol aliyesaini mkataba wa miaka mitano, alifanya vizuri msimu uliopita wa fainali za EURO, ambapo aliwapa wakati mgumu washambuliaji Harry Kane, Rasmus Hojlund, Alexander Mitrovic na Cristiano Ronaldo.
HARRISON ARMSTRONG (EVERTON)
Kiungo raia wa England. Armstrong mwenye umri wa miaka 18, alijiunga na Everton akiwa na umri wa miaka mitano.
Msimu uliopita, nyota huyo alicheza mechi tatu za Ligi Kuu ya England na mkataba wake wa sasa utafikia ukomo mwaka 2028.
CHARALAMPOS KOSTOULAS (BRIGHTON)
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ugiriki ana umri wa miaka 18. Brighton imemng’oa Olympiakos kwa Pauni milioni 30.
Kutokana na uwezo wake mkubwa wa kupachika mabao, mashabiki wa Olympiakos wanamwita ‘Babis-stuta’, wakimfananisha na lejendari wa soka la Argentina, Gabriel Batistuta

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img