MANCHESTER, Uingereza
BAADA ya tetesi za muda mrefu, Manchester United imevunja kibubu na kuchomoa kitita cha Pauni milioni 74 kumsajili mpachikaji mabao wa kimataifa wa Slovenia, Benjamin Sesko, ambaye pia alikuwa kwenye rada za matajiri wa Newcastle United.
Awali, Man United ilimtaka straika wa Aston Villa, Ollie Watkins, kabla ya kuachana na Muingereza huyo na kugeukia kwa Sesko.
Mkurugenzi wa masuala ya usajili, Christopher Vivell, ndiye aliyesimamia dili hilo, akishirikiana na Mkuu wa idara ya takwimu klabuni hapo, Mike Sansoni.
MWENDO WA MABAO TU
Sesko mwenye umri wa miaka 22, alijiunga na RB Leipzig mwaka 2023 akitokea RB Salzburg ya Austria, ambayo pia inamilikiwa na mabosi wa klabu hiyo ya Bundesliga. Usajili huo uligharimu Pauni milioni 20 tu.
Katika msimu wake wa kwanza, Sesko aliingia kambani mara 18 katika mechi 42 za michuano mbalimbali, yakiwamo 14 ya Bundesliga na mawili ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.
Msimu uliopita, ukiwa ni wa pili kwake klabuni hapo, alifunga mabao 21 katika mechi 45, yakiwamo 13 ya Bundesliga. Alipachika manne kwa upande wa Ligi ya Mabingwa.
Tangu alipojiunga na Leipzig, Sesko ndiye mchezaji mwenye umri chini ya miaka 23 aliyefunga mabao mengi zaidi (39) katika Ligi Kuu zote kubwa tano barani Ulaya (England, La Liga, Bundesliga, Serie A na Ligue 1).
MKALI WA MECHI KUBWA
Man United ilihitaji straika wa mechi kubwa. Msimu uliopita, ilifunga mabao sita pekee katika mechi 10 dhidi ya vigogo wengine wa ‘Top Six’.
Sesko ni straika wa daraja hilo. Nyota huyo ameondoka Ujerumani akiwa amefunga mabao matatu katika mechi nne dhidi ya Bayern Munich. Ni wastani wa bao moja kila baada ya dakika 84.
Pia, amepachika mabao matatu na kutoa ‘asisti’ moja katika mechi zake nne alizokutana na Borussia Dortmund.
Itakumbukwa pia, Sesko alitoa asisti wakati Leipzig ilipoibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Bayer Leverkusen iliyokuwa tishio chini ya kocha Xabi Alonso.
Kwa upande wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita, alifunga bao la ugenini dhidi ya Atletico Madrid, pia akiweka mawili dhidi ya Juventus.
AINA YA MABAO YAKE
Katika mabao 27 ya msimu uliopita, Sesko alifunga 15 kwa mguu wa kulia, manne kwa mguu wa kushoto na nane kwa kichwa.
Kwa mabao ya vichwa, ana wastani wa asilimia 29, akiwazidi mastaa kama Alexander Isak (24%), Harry Kane (21%) na Erling Haaland (12%).
Sesko pia ni fundi wa mabao ya mashambulizi ya kushitukiza (counter-attack). Kwa misimu miwili ya hivi karibuni ya Bundesliga, amezidiwa na wachezaji wawili tu (Lois Openda na Omar Marmoush).
Vilevile, mshambuliaji huyo anasifika kwa mabao ya mashuti ya mbali, ambapo amefanya hivyo mara tano, ikiwamo dhidi ya Bayern msimu uliopita.
KUKWEPA MAJANGA YA HOJLUND, ZIRKZEE?
Katika kutafuta suluhisho la ubutu wa safiu yauushambuliaji, Man United ilitumia Pauni milioni 64 kumsajili Rasmus Hojlund mwaka 2022 baada ya kiwango chake bora cha upachikaji mabao akiwa na kikosi cha Atalanta.
Joshua Zirkzee alifuata mwaka mmoja baadaye akiwagharimu matajiri wa Man United kiasi cha Pauni milioni 37 akitokea Bologna.
Hata hivyo, hakuna aliyefaulu kumaliza tatizo. Hojlund amefunga mabao 26 pekee katika mechi 95 alizoshuka dimbani tangu asajiliwe Old Trafford.
Kwa upande wake, Zirkzee aliziona nyavu za wapinzani mara saba pekee katika mechi 49 alizopewa nafasi ya kucheza msimu uliopita (2024-25).
Kutokana na ubutu wao mbele ya lango, Man United ilimaliza msimu ikiwa na Everton, Southampton, Ipswich Town na Leicester City katika orodha ya timu zilizokuwa na idadi ndogo zaidi ya mabao ya kufunga.
Published:


