8.4 C
New York

Arsenal, City, Chelsea nani kuivua ubingwa Liverpool?

Published:

LONDON, England
MARA ya mwisho kwa Liverpool kuchukua mara mbili mfululizo taji la Ligi Kuu ya England (EPL) ni mwaka 1984. Je, watarudia maajabu hayo msimu ujao?
Ikumbukwe, uhondo wa Ligi Kuu hiyo kwa msimu mpya wa 2025-26 unatarajiwa kuanza kuanza Ijumaa ya wiki hii.
Makala haya yanaangazia nafasi ya ‘Majogoo’ wa Anfield kutetea ubingwa, pia wapinzani wao walivyojipanga kuelekea msimu ujao.
LIVERPOOL
Msimu uliopita, ukiwa ni wa kwanza kwa kocha Arne Slot akiwa Anfield, Liverpool ilitwaa ubingwa huo kwa tofauti ya pointi 10 ikiwa na mechi nne mkononi.
Safari hii, kuelekea msimu ujao, kocha Slot ameimarisha kikosi cha matanuzi ya kitita cha Pauni milioni 269 katika soko la usajili la majira haya ya kiangazi.
Katika usajili wake, Slot raia wa Uholanzi ametumia Pauni milioni 100 kuinasa saini ya kiungo aliyetokea Bayer Leverkusen, Florian Wirtz.
Ukiacha usajili huo uliovunja rekodi klabuni hapo, Liverpool imemchukua mpachikaji mabao aliyekuwa Eintracht Frankfurt, Hugo Ekitike, ambaye ameigharimu Pauni milioni 69.
Wakati huo huo, Slot ameimarisha safu ya ulinzi kwa kuwasajili mabeki wa pembeni, Molas Kerkez (Bournemouth) na mwenzake wa kushoto, Jeremie Frimpong (Bayern Leverkusen), na kipa Giorgi Mamardashvili (Valencia).
ARSENAL
Baada ya kushika nafasi ya pili kwa misimu miwili mfululizo, safari hii ni kama Washika Bunduki wameupania zaidi ubingwa wa EPL.
Arsenal si tu haijawa bingwa wa EPL tangu mwaka 2004, bali pia haijabeba taji lolote tangu mwaka 2020.
Katika soko la usajili la majira haya ya kiangazi, kocha Mikel Arteta ameboresha kikosi kwa kuwanasa mastaa sita, akiwamo straika wa viwango kutoka Sporting Lisbon, Viktor Gyokeres.
Wachezaji wapya wengine ni Martin Zubimendi (Real Sociedad), Noni Madueke na Kepa Arrizabalaga (Chelsea), Christian Norgaard (Brentford), na Cristhian Mosquera (Valencia).
Maboresho hayo yameambatana na kuwafungulia mlango wa kutokea wachezaji kama Kieran Tierney, Jorginho, Thomas Partey na Takehiro Tomiyasu.
MANCHESTER CITY
Vijana wa kocha Pep Guardiola walimaliza msimu uliopita wakiwa nafasi ya tatu, wakizidiwa pointi 13 na mabingwa Liverpool.
Kwa mujibu wa historia, mara ya mwisho kwa Man City kumaliza nje ya nafasi mbili za juu ilikuwa mwaka 2017.
Licha ya kuishia hatua ya 16 bora katika fainali za Kombe la Dunia kwa ngazi ya Klabu, bado Guardiola ana kikosi bora, achilia mbali usajili aliofanya wa kuongeza mastaa watano.
Nyota wapya kikosini ni Tijjani Reijnders (AC Milan), Rayan Cherki (Lyon), Rayan Ait-Nouri (Wolves), James Trafford (Burnley) na Sverre Nypan (Rosenborg), ambao wamegharimu Pauni milioni 150.
CHELSEA
Kocha Enzo Maresca naye ana kazi ya kufanya. Msimu uliopita, wakali hao wa Stamford Bridge walimaliza katika nafasi ya nne, wakiwa wameachwa pointi 15 na Liverpool.
Hata hivyo, Chelsea wameonesha kuwa na mabadiliko makubwa. Wametoka kutwaa Kombe la Dunia kwa ngazi ya Klabu wakiifunga PSG mabao 3-0 katika mchezo wa fainali.
Safari hii, kocha Maresca ameimarisha kikosi kwa Pauni milioni 249 alizotumia sokoni kuwapata Liam Delap (Ipswich), Joao Pedro (Brighton), Jamie Gittens (Borussia Dortmund na Jorrel Hato (Ajax).
Nyota hao wataungana na Dario Essugo (Sporting Lisbon) na Estevao Willian (Palmeiras), ambao walishanaswa mapema zaidi.
Pia, tayari kikosi cha Blues kina wachezaji walio kwenye ubora mkubwa, wakiwamo
Cole Palmer, Enzo Fernandez, Moises Caicedo na Marc Cucurella.
NEWCASTLE UNITED
Matajiri wapya wa EPL, Newcastle, wao waliumaliza msimu uliopita wakiwa nafasi ya tano kwenye msimamo. Waliachwa pointi 18 na Liverpool.
Lakini, Newcastle haikumaliza kinyonge msimu huo kwani ilitwaa ubingwa wa Kombe la Ligi (Carabao Cup) kwa ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo wa fainali dhidi ya Liverpool.
Katika kujitafuta kwa ajili ya msimu ujao, mabosi wa klabu hiyo wameshatumia kitita cha Pauni milioni 55 kuwasajili wacheza wawili, Anthony Elanga (Nottingham Forest) na Aaron Ramsdale (Southampton).
Hata hivyo, Newcastle ingeweza kuwa bora zaidi kama si kuzikosa saini za Hugo Ekitike, Joao Pedro, James Trafford, Liam Delap na Dean Huijsen.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img