24.2 C
New York

Nani kati ya mastaa hawa kuibeba Ballon d’Or 2025?

Published:

LONDON, Uingereza

MSIMU uliopita, tuzo maarufu ya Mchezaji Bora wa Mwaka ya jarida la France Football, Ballon d’Or, ilitua mikononi mwa kiungo wa Manchester City na timu ya Taifa ya Hispania, Rodri. Kwa mwaka huu, tayari orodha ya wachezaji 30 wanaoiwania tuzo hivyo imeshaanikwa kuelekea hafla ya kutangaza mshindi itakayofanyika Septemba.

Je, nani ataibuka nayo safari hii? Makala haya yanachambua wachezaji 6 wanaopewa nafasi kubwa ya kuondoka na tuzo hiyo.

OUSMANE DEMBELE (PSG)

Mshambuliaji huyo raia wa Ufaransa anapewa nafasi kubwa baada ya kufanya vizuri msimu uliopita akiwa na vigogo wa Ligue 1, PSG. Dembele aliyefunga mabao 35 na kutoa ‘asisti’ 15, aliiongoza klabu hiyo ya jijini Paris kutwaa mataji matatu; Ligue 1, Kombe la Ligi (Coupe de France) na Ligi ya Mabingwa Ulaya.

LAMINE YAMAL (BARCELONA)

Akiwa na umri wa miaka 18 tu, Yamal anaandika historia ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuingia kwenye kinyang’anyiro cha tuzo hizi za Ballon d’Or. Msimu uliopita ulikuwa mzuri kwa Mhispania huyo, ambapo kikosi chake cha Barcelona kilibeba mataji mawili (Copa del Rey na La Liga) akiwa amefunga mabao 18 na kutoa asisti 20.

RAPHINHA (BARCELONA)

Takwimu za msimu uliopita zinaonesha kuwa hakuna mchezaji wa Barcelona aliyekuwa amemzidi Raphinha kwa mchango wa mabao kikosini. Nyota huyo wa Kibrazil aliyewahi kutikisa Ligi Kuu ya England (EPL) akiwa na Leeds United, alifunga mabao 35 na kutoa asisti 25.

MOHAMED SALAH (LIVERPOOL)

Licha ya kwamba Liverpool haikufika mbali kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, mshambuliaji huyo raia wa Misri alikuwa na mchango mkubwa kwao. Mabao zaidi ya 30, achilia mbali asisti takribani 20, viliifanya Liverpool iwe na ubavu wa kutwaa ubingwa wa EPL.msimu uliopita.

SCOTT MCTOMINAY (NAPOLI)

Kiungo huyo wa kimataifa wa Scotland amekuwa kwenye kiwango bora tangu alipojiunga na Napoli ya Serie A akitokea Manchester United. Msimu uliopita, ukiwa ni wa kwanza, McTominay alifunga mabao 12 na haikushangaza kuona ‘mido’ huyo akitangazwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwaka klabuni hapo.

KHVICHA KVARATSKHELIA (PSG)

Winga wa kimataifa wa Georgia aliyekuwa na mchango mkubwa kwa PSG kumaliza msimu uliopita ikiwa na mataji matatu mkononi. Kvaratskhelia aliyewahi kukipiga Serie A akiwa na Napoli, alichangia mabao zaidi ya 25, akisaidiana na Dembele kuwapa wakati mgumu mabeki wa pembeni wa wapinzani wao.

Related articles

Recent articles