LONDON, Uingereza
KWA mujibu wa mtandao maarufu wa takwimu wa Supercomputer, Manchester United na Tottenham zitamaliza vibaya msimu ujao wa Ligi Kuu ya England (EPL).
Si tu kukosa ubingwa, bali pia timu hizo zitamaliza zikiwa nje ya nafasi nne za juu (Top Four), kwa mujibu wa mtandao huo.
Man United ya kocha Ruben Amorim imetabiriwa na mtandao huo kumaliza msimu ikiwa nafasi ya 12, kwamba itakusanya pointi 49 pekee katika mechi zake zote 38.
Wakati huo huo, utabiri unaonesha kuwa uwezekano wa Man United kumaliza ndani ya ‘Top Four’ ni asilimia 2.7 pekee.
Tottenham, kwa mujibu wa ubashiri wa Supercomputer, watamaliza mbio za ubingwa msimu ujao wakiwa nafasi ya 14.
Msimu uliopita, Spurs walimaliza katika nafasi ya 17, ingawa walijfuta machozi kwa kunyakua ubingwa wa Ligi ya Europa walipoifunga Man United katika mtanange wa fainali.
Msimu ujao, ubashiri wa Supercomputer unaonesha kuwa uwezekano wa Spurs kumaliza ndani ya nafasi sita za juu (Top Six) ni asilimia 4.1 pekee.
Kwa upande mwingine, Supercomputer imetabiri kuwa Liverpool itatetea taji lake, huku Arsenal ikishika nafasi ya pili kama ilivyokuwa msimu uliopita.
Baada ya kushika nafasi hiyo kwa misimu miwili mfululizo, safari hii Arsenal imetumia fedha nyingi kwenye soko la usajili, ikiwamo Pauni milioni 63.5 zilizotumika kumnasa straika Viktor Gyokeres.
Kwa mujibu wa mtandao huo, Liverpool ina asilimia 28.5 ya kubeba tena ubingwa wa EPL, wakati Arsenal wana asilimia 24.3 ya kumaliza nafasi ya pili katika msimamo.
Ubashiri huo wa Supercomputer unaziweka Manchester City na Chelsea katika nafasi ya tatu na ya nne, zikifuatiwa na Aston Villa, Newcastle United, Crystal Palace na Brentford.
Mwisho, ubashiri wa Supercomputer umeonesha kuwa Burnley, Leeds United na Sunderland zina nafasi kubwa ya kurejea ‘mchangani’ Championship (Daraja la Kwanza England).
Published:


