LONDON, Uingereza
UKILIWEKA kando jina la Harry Kane, Son Heung-min anaweza kuwa mchezaji bora zaidi kuwahi kutokea katika klabu ya Tottenham kwa miaka ya hivi karibuni.
Miaka yake 10 akiwa Tottenham inajumuhisha mabao yake 173 na ‘asisti’ 101 katika mechi 454, hivyo anaondoka akiwa lejendari wa klabu hiyo na Ligi Kuu ya England (EPL) kwa ujumla.
Son mwenye umri wa miaka 33, anaiacha Spurs ya Kaskazini mwa Jiji la London ikiwa ni miezi mitatu tu imepita tangu alipoiongoza kutwaa taji la Ligi ya Europa.
Mashabiki wa Tottenham watakumbuka kuwa ni ubingwa wao pekee ndani ya miaka 17 ya hivi karibuni. Pia, ikawa ni mara yao ya kwanza kubeba Ligi ya Europa baada ya miaka 50.
ALIMKATAA POCHETTINO
Baada ya kuajiriwa kuinoa Southampton mwaka 2013, Mauricio Pochettino alijaribu kumsajili Son, ambaye wakati huo alikuwa Hamburg ya Ujerumani.
Akiwa na umri wa miaka 20, Son aliikataa ofa ya Muargentina huyo na kutimkia Bayern Leverkusen. Miaka miwili baadaye, akatua Spurs kuungana na Pochettino.
REKODI YA MCHEZAJI GHALI ZAIDI
Aliposajiliwa na Tottenham mwaka 2015 akitokea Leverkusen, Son raia wa Korea Kusini aliweka rekodi ya kuwa mchezaji ghali zaidi katika historia ya soka barani Asia. Alisajiliwa kwa Pauni milioni 22.5, wakati huo akiwa na umri wa miaka 23.
TUZO, MAJONZI
Msimu wa 2021-22, Son alibeba tuzo ya mfungaji bora wa Ligi Kuu ya England akifungana na Mohamed Salah baada ya kila mmoja kuingia kambani mara 23.
Hata hivyo, Son alifunga mabao hayo bila msaada wa penalti, mchezaji pekee baada ya Sadio Mane (2018-19) kutwaa tuzo ya mfungaji bora wa EPL bila ‘tuta’.
Kwa miaka yake 10, Son ameinyakua mara nne tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi wa EPL, pia akiwahi mara tatu kuwa Mchezaji Bora wa Mwaka wa Spurs.
Lakini, zipo kumbukumbu mbaya kwake, ikiwamo ya kupoteza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mbele ya Liverpool mwaka 2019. Ni kama ilivyokuwa dhidi ya Manchester City katika fainali ya Kombe la Ligi (EFL) mwaka 2021.
UFALME WAKE KOREA
Tafiti zilizofanyika zinaonesha kuwa ukiacha wanamuziki wawili wa Pop, BTS na Blackpink, Son ndiye staa anayekubalika zaidi huko kwao, Korea ya Kusini.
Kutokana na ushawishi wake mkubwa, vipo vipindi maalumu vya televisheni vinavyorusha mabao na ‘asisti’ zake tu.
Si hivyo tu, mashabiki wamekuwa wakisafiri kutoka Korea hadi Uingereza kutazama mechi za Spurs, ambapo hununua jezi zaidi ya 700 za Son na kuingia nazo uwanjani.
Katika Mji anaotokea, Chuncheon, umbali wa maili 50 kutoka Mji Mkuu wa Seoul, lipo sanamu la staa huyo.
HATAKI KAZI YA UKOCHA
Katika mahojiano yake, Son amekuwa akisisitiza kuwa hafikirii kufanya kazi ya ukocha wala kubaki kwenye mchezo wa soka baada ya kustaafu.
Kwa upande mwingine, akihojiwa mwaka jana aliporejea likizo nchini Korea, aliweka wazi kuwa nia yake ni kucheza kandanda kwa miaka mingi.
Published:


