KINSHASA, DRC
WIKI iliyopita, watu wenye silaha walioripotiwa kuwa ni wapiganaji wa Kundi la The Allied Democratic Forces (ADF) walivamia kanisa mjini Komanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kuua waumini takribani 43.
Ikumbukwe, kuibuka kwa kasi kwa matukio ya ADF katika miezi ya hivi karibuni kunakuja wakati Serikali ya DRC ikiwa imepiga hatua kubwa ya kurejesha hali ya usalama nchini humo baada ya kusaini mikataba ya amani na Rwanda na wapiganaji wa M23.
Tukio hilo la Mashariki mwa DRC lililoshuhudia watu wengine wakitekwa, limelaaniwa vikali na Serikali ya Marekani na Vatican.
Taarifa rasmi za mamlaka za DRC zinaeleza kuwa wapiganaji hao waliondoka na watoto kadhaa wenye umri kati ya miaka 12 na 14.
Kwa upande mwingine, mamlaka zinaeleza kuwa wapiganaji wa (ADF), mbali ya kuua, kujeruhi na kuteka, pia walichoma moto nyumba na maduka.
Saa chache baada ya tukio, Kundi hilo la ADF liliachia taarifa yao ya kukiri kuhusika kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram.
ADF ni Kundi linalondesha operesheni zake katika mikoa inayoziunganisha DRC na Uganda, likitajwa kushirikiana na ISIS.
Kwa ufupi, ISIS ni Kundi la kigaidi Mashariki mwa Kati, ambalo limekuwa likitekeleza mashambulizi kwa madai ya kutetea masilahi ya Dini ya Uislam.
Wataalamu wanasema baada ya ISIS kukwama katika jitihada zake za kuitawala Mashariki ya Kati, imekuwa ikifadhili vikundi vya kigaidi maeneo mengi duniani, ikiwamo ADF kwa upande wa Afrika.
ADF lilianza kama kikundi cha waasi nchini Uganda mwaka 1994, kikiipinga Serikali kwa madai ya kutokutenda haki dhidi ya waumini wa Dini ya Uislam.
Mwaka 2012, wapiganaji wa ADF walivuka mpaka na kuingia DRC, hatua iliyokuja baada ya kuona wamezidiwa nguvu na wanajeshi wa Uganda.
Wakiwa wameweka makazi yao Kaskazini mwa Mji wa Kivu, ADF waliendeleza mashambulizi yao katika maeneo mbalimbali ya nchi zote mbili (Uganda na DRC).
Kwa sasa, kiongozi mkuu wa Kundi hilo lenye wapiganaji takribani 1,500 ni Musa Seka Bakulu, ambaye vyanzo mbalimbali vya habari vinaripotiwa kuwa ana umri wa miaka 48.
“Lengo la Kundi hili ni kueneza Uislam. Pia, limelenga kuziondolea utulivu Serikali za Uganda na DRC,” anasema Nico Minde, mchambuzi wa masuala ya usalama.
Licha ya kutokuwapo kwa idadi kamili, Minde na wachambuzi wengine wanakubaliana kuwa mashambulizi ya ADF yameshaua watu takribani 1,000 kwa kipindi cha miaka 30 iliyopita.
Mwanzoni mwa mwezi uliopita, ADF iliua watu 41 katika mashambulizi yake mjini Ituri. Kabla ya tukio hilo, ilishaua 18 mjini Babili na wengine 41 huko Lubero.
Ni kutokana na takwimu hizo za mauaji yalioambatana na utekaji, mwaka 2021, Serikali ya Marekani iliitaja ADF kuwa ni kikundi cha kigaidi hatari zaidi barani Afrika.
Katika mapambano dhidi ya ADF, DRC haiko peke yake. Serikali ya Uganda imekuwa ikionesha jitihada kubwa kukabiliana na Kundi hilo.
Hiyo ni pamoja na kupeleka wanajeshi takribani 4,000 nchini DRC, wakishirikiana na wale wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa (MONUSCO).
Kupitia operesheni waliyoiita ‘Operation Shujaa’, jitihada hizo zimesababisha kutiwa nguvuni kwa viongozi waandamizi wawili wa Kundi la ADF.
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa siasa wamekuwa wakiinyooshea kidole Uganda kwa madai ya kutumia mgogoro huo kama fursa ya kuingia DRC na kuiba rasilimali za nchi hiyo.
Uganda ni mshirika mkubwa wa kibiashara wa DRC. Kwa mujibu wa Msemaji wa jeshi la Uganda, Felix Kulayigye, kuingia kwao DRC ni katika kulinda masilahi ya kibiashara kati ya mataifa hayo.
Lakini, hii si mara ya kwanza kwa Uganda kuhusishwa na wizi wa rasilimali za DRC. Ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa imewahi kuitaja kufadhili Kundi la M23 huko Mashariki mwa DRC.
Ni wakati huo pia, hata Mkuu wa Jeshi la Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, alikiri kupitia mtandao wa ‘X’ kuwa wanaiunga mkono M23.
Published:


