13.9 C
New York

Kagera yafanya mageuzi makubwa ya maendeleo

Published:

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

Mkoa wa Kagera umeandika historia mpya ya maendeleo kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi Aprili 2025, kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati iliyoboresha sekta za afya, elimu, maji, nishati, kilimo, biashara na miundombinu kwa kiwango kikubwa.

Akizungumza jijini Dodoma leo Julai 1, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa, alisema mafanikio hayo yametokana na dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, pamoja na ushirikiano imara wa wananchi, viongozi na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Sekta ya Afya

Mwassa alisema moja ya mafanikio makubwa ni ongezeko la vituo vya kutolea huduma za afya, ambapo hospitali za wilaya zimeongezeka kutoka 3 hadi 11, vituo vya afya kutoka 29 hadi 42, na zahanati kutoka 217 hadi 283.

Aidha, huduma za kibingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa zimeboreshwa na kuongeza idadi ya wagonjwa waliotibiwa ndani ya mkoa kwa asilimia 273, hatua iliyopunguza kwa kiasi kikubwa utegemezi wa rufaa kwenda Mwanza na Dar es Salaam.

“Huduma za upasuaji wa pua, koo na masikio, mifupa na magonjwa ya ndani zimeleta mapinduzi makubwa katika huduma za afya kwa wananchi wa Kagera,” alisema.

Sekta ya Elimu

Katika sekta ya elimu, Mwassa alieleza kuwa shule mpya 116 za awali na msingi, pamoja na shule 68 za sekondari zimejengwa, sambamba na vyuo vya ufundi stadi (VETA) vitano. Vituo vya elimu vimeongezeka kutoka 4 hadi 9, ikiwemo Chuo cha VETA Burugo kilichogharimu zaidi ya shilingi bilioni 20.

Aidha, vyumba vya madarasa 4,709, maabara 167 na mabweni 121 vimejengwa, hatua iliyopunguza kwa kiasi kikubwa upungufu wa miundombinu mashuleni.

“Ufaulu wa kitaaluma umeimarika, ambapo ufaulu wa kidato cha nne umeongezeka kutoka asilimia 91 hadi 94.57, ikionyesha mafanikio makubwa katika sekta ya elimu,” aliongeza Mwassa.

Kwa ujumla, Mkuu huyo wa Mkoa alisema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo kuhakikisha miradi ya kimkakati inaendelea kuboresha maisha ya wananchi wa Kagera kwa ufanisi zaidi.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img