13.9 C
New York

RC Mtambi aagiza Halmashauri Serengeti kutoa fedha za uendeshaji kwa kila kijiji

Published:

Na Malima Lubasha, Gazetini-Serengeti

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ameielekeza Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kutenga na kupeleka angalau Shilingi 100,000 kila robo mwaka kwa kila kijiji, kwa ajili ya shughuli za uendeshaji wa ofisi za vijiji.

Agizo hilo amelitoa Juni 16, 2025, wakati wa kikao maalum cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kilichofanyika kwa ajili ya kupokea na kujadili Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

“Fedha hizo zitasaidia sana ofisi za vijiji katika shughuli za kila siku. Ni muhimu kuhakikisha kuwa ukusanyaji wa mapato ya ndani unaimarishwa ili kufanikisha hili,” alisema Kanali Mtambi.

Aidha, ameitaka menejimenti ya halmashauri hiyo kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu, hasa kipindi hiki ambacho Baraza la Madiwani linakaribia kuvunjwa.

Pia ameelekeza kuanzishwa na kuimarishwa kwa kitengo cha ufuatiliaji na tathmini ili kiweze kufuatilia utekelezaji wa miradi kwa ufanisi. Alisisitiza kuwa hilo linawezekana endapo kutakuwa na usimamizi mzuri wa vyanzo vya mapato vilivyopo na kuibuliwa kwa vipya.

“Baada ya Baraza kuvunjwa, mtarejea kwenye kata zenu kuwaeleza wananchi mliyowatumikia utekelezaji wa miradi. Natumaini mtarudi tena na kuendelea kuleta maendeleo,” alisema RC Mtambi.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Serengeti, watumishi kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa, maofisa wa CAG na menejimenti ya halmashauri.

Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ina jumla ya vijiji 78 katika tarafa nne za Rogoro, Grumeti, Ikorongo na Ngoreme, ambapo miradi mbalimbali ya maendeleo inaendelea kutekelezwa.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img