Na Jonathan Benedict, Gazetini
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeweka dhamira ya dhati ya kuimarisha ulinzi, malezi na maendeleo ya watoto kupitia Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2025 hadi 2030, kwa kutambua kuwa familia ni msingi wa Taifa na watoto ni kundi linalohitaji uangalizi wa kipekee ili kufikia usawa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kupitia Ilani hiyo, CCM kimeielekeza Serikali kuchukua hatua mbalimbali zenye lengo la kuhakikisha watoto wa Tanzania wanalelewa katika mazingira salama, yenye maadili na yenye kuwajengea uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maisha ya baadaye.
Miongoni mwa maeneo yanayopatiwa kipaumbele ni pamoja na kudhibiti ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto katika kaya, taasisi za elimu, vituo vya malezi, na maeneo ya umma na binafsi. Ilani hiyo inasisitiza umuhimu wa kujenga jamii inayowajibika kwa kuhakikisha watoto wanalindwa dhidi ya vitendo vyote vya ukatili na manyanyaso.
Vilevile, CCM imejipanga kuimarisha misingi ya familia bora kwa kusisitiza malezi yenye kuzingatia maadili ya Kitanzania. Lengo ni kujenga jamii imara na yenye mshikamano, ambapo familia zinabeba jukumu la msingi katika makuzi ya watoto wao.
Katika kuhakikisha usawa wa kijinsia, Ilani imeweka bayana kuwa masuala ya jinsia yatalindwa na kuzingatiwa katika sera, mipango na miradi ya maendeleo ili kuhakikisha watoto wa jinsia zote wanapata fursa sawa katika maeneo yote ya maisha.
Kadhalika, CCM imeweka msisitizo mkubwa katika kuimarisha huduma za malezi na makuzi ya awali ya watoto, kuhakikisha wanapata huduma bora kuanzia hatua za mwanzo za maisha yao. Hii inajumuisha lishe bora, afya, elimu ya awali na ustawi wa kijamii unaowawezesha kukua katika mazingira yenye fursa na ulinzi wa kutosha.
Ilani hii inaakisi dhamira ya CCM ya kujenga Taifa lenye usawa, haki na maendeleo jumuishi kwa kuhakikisha kundi la watoto, ambalo ndilo nguzo ya baadaye ya Taifa, linapata uangalizi na uwezeshaji unaostahili katika kila hatua ya ukuaji wao.