21 C
New York

Elimu bila malipo kuendelea, kuboresha mazingira ya wanafunzi 2025–2030

Published:

Na Jonathan Benedict, Gazetini

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2025–2030, kimeweka mkazo mkubwa katika kuboresha maisha ya watoto wa Kitanzania kupitia sekta ya elimu, kwa kuahidi kuendeleza utoaji wa elimu bila ada kuanzia ngazi ya awali hadi kidato cha sita.

Katika kipindi cha miaka minne iliyopita (2020–2024), Serikali chini ya uongozi wa CCM imetumia jumla ya Sh trilioni 1.3 kugharimia elimu bila ada, hatua iliyochangia mafanikio makubwa katika upatikanaji wa elimu kwa watoto wengi nchini.

Taarifa kutoka ndani ya Ilani hiyo inaeleza kuwa mafanikio hayo ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi waliosajiliwa katika elimu ya awali kutoka 1,278,886 mwaka 2020 hadi 1,558,549 mwaka 2024, huku usajili wa wanafunzi wa darasa la kwanza ukiongezeka kutoka 1,621,482 hadi 1,862,539 kwa kipindi hicho.

Aidha, wanafunzi waliojiunga na kidato cha kwanza wameongezeka kutoka 722,893 mwaka 2020 hadi 1,056,789 mwaka 2024, na kidato cha tano kutoka 78,434 hadi 127,008. Kwa ujumla, hatua hizo zimechochea ongezeko la wanafunzi wanaojiunga na elimu ya sekondari kufikia asilimia 70.

CCM pia imeeleza kuwa katika kipindi hicho, wanafunzi wa kike 10,864 walirejeshwa shuleni baada ya kukatisha masomo yao, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha watoto wote wanapata haki sawa ya elimu bila vikwazo vya kijinsia au kijamii.

Kwa upande wa elimu ya juu, wanafunzi waliodahiliwa waliongezeka kutoka 233,734 mwaka 2020 hadi 334,854 mwaka 2024, ikiwa ni ongezeko la asilimia 43.3. Idadi ya wanafunzi waliopata mikopo iliongezeka kutoka 142,170 hadi 245,799 katika kipindi hicho hicho.

Katika kuhakikisha wanafunzi wengi zaidi wanapata fursa ya kusoma, Serikali ilitumia jumla ya Sh. trilioni 2.76 kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kati ya mwaka wa fedha 2021/22 hadi 2024/25.

Kwa mara ya kwanza, Serikali imeanza pia kutoa mikopo kwa wanafunzi wa ngazi ya stashahada, ambapo wanafunzi 9,959 wamenufaika na mikopo hiyo katika fani zenye kipaumbele ikiwemo afya, kilimo, usafirishaji, ualimu wa ufundi, ufundi stadi na uhandisi wa nishati na madini.

Sambamba na hilo, Serikali imeanzisha Samia Scholarship, mpango wa kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi mahiri, ambapo hadi kufikia mwaka 2024, wanafunzi 3,696 walikuwa wamefaidika na mpango huo.

Kwa mujibu wa Ilani hiyo, hatua nyingine kubwa iliyochukuliwa ni kuhuisha Sera ya Taifa ya Elimu na Mafunzo pamoja na mitaala yake ili kutoa wahitimu bora, mahiri na wenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya soko la ajira la sasa na baadaye.

Katika upande wa matokeo ya mitihani, kiwango cha ufaulu kwa darasa la saba kilifikia asilimia 80.6 mwaka 2023, ufaulu wa kidato cha nne uliongezeka kutoka asilimia 85.8 mwaka 2020 hadi asilimia 89.37 mwaka 2023, huku ufaulu wa kidato cha sita ukifikia asilimia 99.9 mwaka 2024.

Kupitia Ilani ya 2025–2030, CCM imejipanga kuendeleza mafanikio haya na kuongeza kasi ya uwekezaji katika elimu ili kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata fursa ya kusoma, kufaulu na kuchangia maendeleo ya taifa.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img