3.7 C
New York

Mabondia wamchana ‘live’ Amos Mwamakula baada ya kushindwa kesi ya Vitasa na Azam Media

Published:

Na Mwandishi Wetu

Mabondia wa ngumi za kulipwa nchini wamefurahia kitendo cha Azam Media kushinda Rufaa ya kesi ya Vitasa, huku wakikemea kitendo alichofanya bondia mkongwe Amos Mwamakula kwa kuifungulia kesi kampuni hiyo Mahakamani kwani ndiyo ilikuwa mhimili wao wa kujipatia kipato.

Mwamakula aliifungulia kesi Azam Media kwa madai ya haki miliki ya jina la Vitasa linalotumiwa katika kurusha matangazo ya ngumi.

Wakizungumza na waandishi wa habari leo Mei 27, 2025, jijini Dar es Salaam, mabondia Ibrahim Class, Mfaume Mfaume, Dulla Mbabe, Nasibu Ramadhani na wengine wamesema hawataweza kumsamehe Mwamakula kwa sababu amewafanya mabondia wengi kuishi maisha magumu mtaani, huku vipaji vipya vikishindwa kuonekana.

Aidha wameiomba Azam Media irejee kuonesha mapambano ya ngumi, ili kuendelea kuinua vipaji na kukuza vipato vyao kwani ndiyo kazi wanayotegemea.

“Tulipitia kipindi kigumu. Mimi binafsi nilikata tamaa hadi nikaacha kufanya mazoezi. Lakini sasa, baada ya Azam kushinda kesi, nimepata nguvu upya na nimerudi mazoezini,” amesema Mfaume Mfaume.

Kwa upande wake, Ibrahim Class amesema Azam TV iliwasaidia sana kujulikana na kupata mafanikio alafu anatokea mtu anakwenda kufungua kesi na kuwaumiza wengine.

“Kitendo alichofanya hata kama alikuwa ni rafiki yangu siwezi kumsamehe kwa sababu amewafanya mabondia wawe na njaa mtaani, tunakosa mapambano,” amesema Class.

Naye Abdallah Pazi ‘Dulla Mbabe’ alisema kutokana na hali ilivyokuwa baadhi walirudi katika kazi zao za zamani ambazo ni ngumu hata kuzielezea lakini anashukuru uamuzi wa Mahakama, akiamini mambo yatakuwa sawa hivi karibuni.

“Kipindi Azam wanarusha ngumi, ilitusaidia sana hadi wengine tumepata ubalozi wa makampuni mbalimbali tunaingiza hela. Tunaomba Azam warudi, tuanze tena mapambano, hata tukianzia sisi kwa sisi kwanza asiwepo bondia wa nje,” amesema Dulla Mbabe.

Bondia chipukizi Rahim Omar amesema vijana wengi walikuwa wamekata tamaa kwa kuwa Azam ilionekana kuwa njia yao ya mafanikio.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img