17.6 C
New York

Nane kuamua ubingwa daraja la nne Nyamagana, Mabula agawa vifaa

Published:

Na Mwandishi wetu, Mwanza

Timu nane zilizofuzu hatua ya robo fainali (Super 8) itakayochezwa kwa mtindo wa mzunguko zinatarajia kuamua bingwa wa michuano ya Ligi Daraja la Nne Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza atakayewakilisha kwenye ligi daraja la tatu mkoani hapa.

Timu hizo ni Bocca Juniors, Liberty FC, Nyamwaga, FC Tiger, Mwanza City, Mzalendo FC, Nyamagana Sport, na Lake Tiger ambapo mechi za hatua hiyo zitachezwa Uwanja wa Nyamagana kuanzia Mei 13 hadi 26, mwaka huu.

Baadhi ya wawakilishi wa timu zilizofuzu nane bora ya Ligi Daraja la Nne Wilaya ya Nyamagana wakipokea jezi kutoka kwa Maxwell Mabula ambaye ni mwakilishi wa Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, Stanslaus Mabula. Picha na Mpiga picha wetu

Mdhamini wa ligi hiyo, Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, Stanslaus Mabula amekkabidhi jezi pea moja kwa timu hizo nane kuhakikisha zinashiriki hatua hiyo bila changamoto zozote huku akiahidi kuendelea kudhamini mashindano hayo.

Akizungumza juzi wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa hivyo, Mwenyekiti wa Chama cha Soka Wilaya ya Nyamagana (NDFA), Said Kizota alisema lengo ni kupata bingwa atakayekwenda kuwakilisha vyema kwenye ligi ya mkoa na kuendelea ubabe wa wilaya hiyo kwenye mashindano hayo.

“Tunamshukuru Stanslaus Mabula (Mbunge) amekuwa mdhamini wetu kwa miaka 10 akitusaidia vifaa (jezi), posho na zawadi kwa washindi, imetusaidia kuboresha mashindano yetu na kutufanya kuwa wilaya ambayo inazalisha ligi bora,” amesema Kizota.

Ameongeza kuwa; “Kwa misimu nane mfululizo bingwa wa Ligi ya Mkoa ametoa wilaya ya Nyamagana na katika hicho kipindi timu zote zinazokutana fainali ya ligi ya mkoa zinatoka Nyamagana, kwahiyo inaonyesha namna gani tumedhamiria kuwa washindani.”

Katibu wa NDFA, William Malagila alisema kutokana na uhaba wa viwanja wanatarajia kutumia uwanja wa Nyamagana kwa mechi za awali, huku uwepo wa mvua, changamoto za usafiri na wachezaji wengi kuwa wanafunzi kukiathiri mashindano hayo.

“Mizunguko mitatu ya kwanza tutacheza Nyamagana mpaka hapo ratiba nyingine itakapofuata, ratiba yetu imebanana kutokana na changamoto za usafiri, mvua, na wachezaji wengi kuwa ni wanafunzi kwani mashindano ya Umisseta na Umitashumta yameanza,” alisema Malagila.

Naye, Maxwell Mabula akizungumza kwa niaba ya Mbunge Stanslaus Mabula,  aliupongeza uongozi wa NDFA kwa usimamizi makini wa ligi hiyo na kuweka imani kwa mbunge, Stanslaus Mabula kuwekeza nguvu na fedha kwa miaka 10 mfululizo, huku akiahidi kuendelea kuiunga mkono michuano hiyo.

Naye, Nahodha wa Lake Tiger FC, Baraka Samwel ‘Modeste’ alisema wamejiandaa vizuri kutoa ushindani kuhakikisha wanatwaa ubingwa, huku Nahodha wa Tiger FC, Michael Jospeh ambaye timu yake inashiriki michuano hiyo kwa msimu wa pili akitamba kuwa wameshapata uzoefu wa kutosha kuwawezesha kutwaa ubingwa.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img