HATIMAYE dirisha kubwa la usajili ambalo aghalabu hufanyika majira ya kiangazi barani Ulaya, lilifungwa hivi karibuni (Agosti 31). Mengi yalishuhudiwa, kubwa ikiwa ni Lionel Messi kwenda PSG akitokea Barcelona, pia Cristiano Ronaldo akirejea Old Trafford.
Itoshe kusema harakati zote zilikwisha huku klabu za Ligi Kuu England zikiwa zimesajili wachezaji 148, wakiwamo waliochukuliwa kwa mkopo. Ni idadi kubwa ukilinganisha na mwaka jana walipokuwa 132.
Lakini je, yapi mengine yaliyohitimisha dirisha la usajili lililokuwa wazi kwa miezi miwili? Makala haya yanakuchimbulia…
EPL yaziburuza Serie A, La Liga
Kwa mujibu wa mtandao wa Deloitte, klabu za Ligi Kuu England (EPL) ilitumia fedha nyingi kununua wachezaji kuliko ligi zingine nne kubwa za Ulaya. Kwamba EPL ilitumia Pauni bilioni 1.1 (Tsh tril. 3.5), ikifuatiwa na Serie A iliyokuwa na Pauni milioni 475 (Sh bil. 1.5).
Nafasi ya tatu ilishikwa na Bundesliga (Pauni mil. 360 – Tsh Bil. 1.1), Ligue 1 (Pauni mil. 325 – Tsh bil. 1) na La Liga (Pauni mil. 250 – Tsh Bil. 790).
Hata hivyo, kwa EPL bado ni anguko kubwa kwani utumizi wa fedha kwenye usajili umeshuka kwa asilimia 11, ukilinganisha na soko la usajili wa kiangazi, mwaka jana.
Usajili huu wa kiangazi ulishuhudia klabu za Ligi Kuu zikisajili wachezaji sita tu kutoka ligi za chini, tofauti na 22 waliopata ‘zali’ mwaka jana.
Wakali wa bei mbaya
Zilifanyika dili nyingi lakini ni wachezaji wanne tu waliosajiliwa kwa ada ya Pauni milioni 50 (Tsh bil. 159) au zaidi. Katika orodha hiyo ni Ben White (Arsenal, Pauni mil. 50), Jadon Sancho (Man United, Pauni mil. 73 – Tsh bil 233), Romelu Lukaku (Chelsea, Pauni mil. 97.5 – Tsh bil. 310), na Jack Grealish (Man City, Pauni mil. 100 – Tsh bil. 320).
Kwa upande mwingine, walionaswa kwa Pauni milioni 10 hadi Pauni milioni 25 walikuwa 33. Msimu uliopita walikuwa 20.
Arsenal kinara matumizi England
Arsenal ilikuwa kinara kwenye utumizi kwa upande wa EPL kwani ilimwaga sokoni Pauni milioni 149 (Tsh bil. 477). Man United ilishika nafasi ya pili kwa Pauni milioni 126 (Tsh bil 403). Man City ilitumbua Pauni milioni 106 (Tsh bil. 339), huku Chelsea ikifuatwa na Pauni milioni 108 (Tsh bil. 346).
Orodha hiyo ya timu tano inakamilishwa na Tottenham waliotumia Pauni milioni 60 (Tsh bil. 193). Liverpool ilisajili mchezaji mmoja tu, Ibrahima Konate, ikitumia Pauni milioni 35 (Tsh bil. 113).