HIVI karibuni Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta, alitua kwa mkopo Royal Antwerp ya Ubelgiji akitokea Fenerbahce ya Ligi Kuu nchini Uturuki.
Ifahamike kuwa Samatta ameondoka Uturuki akiwa ameifungia Fenerbahce mabao matano pekee katika mechi 27 alizocheza tangu alipojiunga nayo mwaka juzi akitokea Aston Villa.
Kabla ya kujiunga na Royal Antwerp, saini ya Samatta ilikuwa ikiwaniwa na klabu mbili za Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1); Troyes na Montpellier.
Royal Antwerp wana rekodi gani?
Ilianzishwa mwaka 1880 na inatajwa kuwa ndiyo klabu kongwe zaidi katika historia ya soka la Ubelgiji. Royal Antwerp imetwaa mara nne ubingwa wa Ligi Kuu, pia ikiibeba mara tatu ‘ndoo’ ya Kombe la Ligi.
Hata hivyo, hawajawa mabingwa wa Ligi Kuu tangu mwaka 1957 na walipotea kwenye ligi kwa miaka 13 kabla ya kurejea mwaka 2017.
Aidha, klabu hiyo ina ushirikiano wa karibu na Man United kwani zimekuwa zikibadilishana makinda. Mahasimu wao wakubwa ni Beerschot A.C na mara nyingi wanapokutana nao huwa zinatokea fujo za mashabiki.
Hali yao ikoje kwenye ligi?
Msimu uliopita, walimaliza ligi kwenye nafasi ya nne, wakiachwa pointi 17 na mabingwa Club Brugge. Katika mechi tano za msimu huu, bado mambo si mazuri kwao. Wameshinda moja, wamefungwa mbili na sare mbili, hivyo wako nafasi ya 15 kwenye msimamo.
Mbali ya Samatta, Royal Antwerp imeongeza idadi ya Waafrika kikosini kwani tayari ina wengine sita; Abdoulaye Seck (Senegal), Alhassan Yusuf (Nigeria), Nill De Pauw (Congo), Luete Ava Dongo (Congo), Bruny Nsimba (Angola) na Opoku Ampomah (Ghana).
Pia, ndani ya kikosi hicho anakwenda kukutana na kiungo mkongwe aliyewahi kutamba Ligi Kuu ya Italia (Serie A) akiwa na klabu za Inter Milan na AS Roma, Radja Nainggolan.
Kwanini hakwenda Ufaransa?
Kwa mujibu wa taarifa, ofa iliyowekwa mezani na Royal Antwerp ilikuwa ‘bab kubwa’, ukilinganisha na klabu zingine. Chanzo cha kuaminika kinasema Royal Antwerp waliweka mezani euro milioni nne (zaidi ya Sh bil. 10 za Tanzania), wakati Montpellier iliishia euro milioni 2.5 (zaidi ya Sh bil. 6).
Samatta atarudisha heshima Ubelgiji?
Kwa mara ya kwanza, Samatta aliingia Ubelgiji mwaka 2016 na kuiunga na Genk akitokea TP Mazembe. Akiwa na timu hiyo kwa misimu minne, alifunga mabao 76 na ‘asisti’ 20 katika mechi 191.
Kiwango hicho kilimpa nafasi ya kusajiliwa Aston Villa kwa mkataba wa miaka minne na nusu lakini alifunga mabao mawili pekee katika mechi 16.