5.7 C
New York

Mgombea Ubunge CUF auawa, INEC yasitisha kampeni za ubunge

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

Mgombea ubunge wa Jimbo la Siha, kupitia Chama cha Wananchi (CUF) mkoani Kilimanjaro, Daudi Ntuyehabi ameuawa na wananchi baada ya kudaiwa kumchoma mwenzake kisu, Abdul Mohamed wakati akiamua ugomvi wa mgombea ubunge huyo na kijana mwingine ambaye waliyekuwa wakidaiana fedha kwenye ‘grocery’ inayouza vinywaji.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema tukio hilo limetokea jana usiku, Oktoba 7, 2025 katika Kijiji cha Kilingi, wilayani Siha.

Kufuatia tukio hilo, watu wanane wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa tuhuma za kujichukulia sheria mkononi kwa kumshambulia mgombea ubunge huyo na kumsababishia kifo.

Kamanda Maigwa amewataja wanaoshikiliwa kuwa ni, Hamadi Issah Mohamed, Alphonce Kinyaha, Rizik Amedeus, Frank Paulo Lutindi, Shedrack Emanuel, Jeremia Mnkondo, Zainab Elisha na Issah Mohamed.

Aidha, Kamanda Maigwa amesema bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio la kuuawa kwa mgombea ubunge huyo.

“Mauaji hayo yametokea Oktoba 7, saa 1:30 usiku katika Kijiji cha Kilingi Sanya Juu, baada ya mgombea ubunge huyo (marehemu) kumchoma kwa kisu tumboni na kusababisha utumbo kutoka nje Abdul Issah Mohamed, Mkazi wa Kilingi,” amesema.

Amesema, “Mohamed bado anaendelea na matibabu hospitalini na inadaiwa sababu za kuchomwa kisu ni kitendo chake cha kwenda kuamua ugomvi uliozuka kati ya Daudi Wilbard Ntuyehabi (marehemu) na Hamadi Issa Mohamed wakati wana kunywa pombe kwenye ‘grocery’ kutokana na kudaiana fedha.”

Katika hatua nyingine, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imesitisha Kampeni za Uchaguzi wa kiti Ubunge katika Jimbo la Siha,  kutokana na tukio hilo

Taarifa kwa umma ya kusitisha uchaguzi wa Ubunge, Jimbo hilo, iliyotolewa na kusainiwa leo Oktoba 8,2025 na Msimamizi wa Uchaguzi, Jimbo la Siha, Marco Masue, inaeleza kuwa kutokana na kutokea kwa tukio hilo, Uchaguzi wa Ubunge katika Jimbo la Siha, umesitishwa kuanzia leo.

 “Kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 71 (1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Namba 1 ya Mwaka 2024, na kwa barua ya tarehe 8, Oktoba 2025 isiyokuwa na kumbukumbu namba kutoka kwa Katibu wa Chama cha Wananchi (CUF), Wilaya ya Siha.

 “Nimepokea taarifa ya kifo cha Ndugu, Daud Wilbrod Ntuyehabi, aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Ubunge, Jimbo la Siha, kupitia Chama cha Wananchi (CUF).

Kutokana na kutokea kwa tukio hilo, Uchaguzi wa Ubunge katika Jimbo la Siha, Wilaya ya Siha, umesitishwa kuanzia leo tarehe 08 Oktoba 2025,” imesema taarifa hiyo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img