LONDON, Uingereza
NI takribani wiki mbili pekee zimebaki kabla ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya England (EPL) kuanza.
Msimu uliopita, makocha nane walifungashiwa virago, wa kwanza akiwa ni Erik ten Hag aliyefukuzwa na Manchester United mwishoni mwa mwaka jana.
Baada ya Ten Hag, makocha wengine waliotimuliwa ni Steve Cooper (Leicester City), Gary O’Neil (Wolves) na Russell Martin (Southampton).
Makocha hao walifuatiwa na Julen Lopetegui, Sean Dyche na Ivan Juric ambaye alikuwa kocha wa pili kufukuzwa na Southampton.
Mambo yalikuwa mabaya pia kwa Ange Postecoglou, aliyefukuzwa licha ya kuipa Tottenham taji la Ligi ya Europa.
Safari hii, kocha aliye kwenye presha kubwa zaidi ni Daniel Farke wa Leeds United, licha ya kazi yake nzuri ya kuirejesha timu hiyo EPL.
Farke ana rekodi mbovu kwenye maisha yake akiwa Ligi Kuu. Msimu wa 2019-20, ambapo aliishusha Daraja klabu ya Norwich City baada ya kushinda mechi tano msimu huo.
Kwa takwimu, ameshinda mara sita pekee katika mechi 49 za EPL, akifungwa 35 na kukusanya pointi 26.
Wakati huo huo, kocha wa Brentford, Keith Andrews, naye hayuko salama kuelekea msimu ujao. Kocha huyo ameajiriwa Brentford kuchukua nafasi ya Thomas Frank aliyetua Tottenham.
Andrews (44), ambaye aliwahi kuinoa Sheffield United, atakuwa na wakati mgumu kwani amekikuta kikosi kikiwa kimewapoteza wachezaji wake muhimu.
Kiungo Christian Norgaard ametua Arsenal, wakati aliyekuwa mshambuliaji tegemeo zaidi kikosini, Bryan Mbeumo, ametimkia Manchester United.
Presha ni kubwa pia kwa kocha wa Sunderland, Regis Le Bris, ambaye si tu hana uzoefu wa EPL, bali pia Sunderland yake imerejea Ligi Kuu kwa ‘play off’ ikiwa imeachwa pointi 24 na Burnley na Leeds.
Published:


