KAMPALA, Uganda
RAIS wa Uganda, Yoweri Museveni, ameweka wazi mpango wake wa kugombea nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mapema mwakani.
Rais Museveni, ambaye sasa ana umri wa miaka 80, amekuwa madarakani tangu mwaka 1986, licha ya kupingwa na wakosoaji wake kwa kile wanachokitaja kuwa ni udikteta.
Wakati huo huo, wanaharakati nchini Uganda na wenzao wa jumuhiya za kimataifa walipinga vikali hatua ya Serikali yake kubadilisha mara mbili Katiba ya Uganda ili tu mwanasiasa huyo aweze kugombea urais.
Watetezi wa haki za binadamu nao wamekuwa mstari wa mbele kuunyooshea vidole utawala wa Rais Museveni wakidai kuwa umekuwa kandamizi dhidi ya wakosoaji, hasa wanasiasa wa upinzani.
Kwa Uchaguzi wa Januari, mwakani, mpinzani wa karibu wa Rais Museveni ni mwanamuziki aliyegeukia siasa, Bobi Wine, ambaye alishika nafasi ya pili mwaka 2021.


