4.5 C
New York

Dawa za kulevya, imani potofu chanzo cha ukatili

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini – RUNGWE

MALEZI duni ndani ya familia, matumizi ya dawa za kulevya na mifumo dume ni miongoni mwa changamoto zinazotajwa kuchangia vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana katika Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya.

Hali hiyo imeelezwa kuhitaji ushiriki wa familia na jamii kwa ujumla katika kuimarisha malezi, kutoa elimu na kuhakikisha wanawake na watoto wa kike wanalindwa dhidi ya vitendo vya ukatili.

Akizungumza na Gazetini baada ya kufungua kikao cha watetezi wa haki za wanawake na wasichana kilichowakutanisha wawakilishi wa asasi za kiraia wilayani humo, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Rungwe, Teddy Siame, amesema watoto wanaokosa malezi bora katika familia huwa katika hatari ya kuingia mikononi mwa watu wenye nia ovu.

“Watoto wakikosa malezi sahihi katika familia huangukia kwenye mikono ya watu waovu, ambao wanaweza kuwafanyia vitendo vya ukatili,” amesema Siame.

Amesema elimu kwa jamii inapaswa kutolewa mara kwa mara ili kuongeza uelewa na kusaidia kupunguza vitendo hivyo, huku akieleza kuwa mifumo dume nayo inaendelea kuathiri nafasi ya wanawake katika kufanya maamuzi kuhusu mali wanazozalisha.

Kwa mujibu wa Siame, wanawake wengi katika Wilaya ya Rungwe wanashiriki katika shughuli za kutafuta na kuzalisha mali, lakini hawana mamlaka yanayolingana na mchango wao katika kufanya maamuzi kuhusu mali hizo.

Amesema hali hiyo inaonesha umuhimu wa kuendelea kuelimisha jamii kuhusu haki za wanawake na usawa katika maamuzi ya kiuchumi na kijamii.

Awali, akifungua kikao hicho, Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Elimisha, Debora Mwanyanje, amesema shirika hilo linaunga mkono juhudi za Serikali katika kupambana na ukatili kwa kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu madhara ya vitendo hivyo.

Mwanyanje amesema matarajio ya asasi za kiraia zinazotetea haki za wanawake na watoto wa kike ni kuona jamii ikibadilika na kuachana na vitendo vya ukatili.

Amesisitiza kuwa ulinzi wa watoto dhidi ya vitendo hivyo si jukumu la Serikali au asasi za kiraia pekee, bali ni wajibu wa kila mwanajamii.

Kwa upande wao, washiriki wa kikao hicho, Ezron Kyejo, Festina Mwakipunga, Victor Mwaigwisya na Maria Petter, wameitaka jamii kushiriki kikamilifu katika kuwalinda wanawake na wasichana, huku wakihimiza wananchi kutoa taarifa za vitendo vya ukatili kwa mamlaka husika ili hatua stahiki zichukuliwe.

Shirika la Elimisha lilianzishwa na baadhi ya waandishi wa habari mkoani Mbeya mwaka 2009 na kusajiliwa mwaka 2010, likiwa na lengo la kutoa elimu kwa jamii kuhusu vitendo vya ukatili na kuhamasisha mapambano dhidi ya tatizo hilo.

Related articles

Recent articles