CAIRO, Misri
SHIRIKISHO la Soka barani Afrika [CAF] limeanika majina ya mastaa watano wanaowania tuzo ya Mchezaji Bora wa mwaka 2026. Nyota hao ni Sadio Mane, Pape Gueye, Achraf Hakimi, Brahim Diaz na Ismael Saibari.
Mshindi wa tuzo hiyo, ambayo kwa sasa inashikiliwa na Hakimi, anatarajiwa kutangazwa kupitia hafla itakayofanyika mjini Lagos, Nigeria.
Hata hivyo, imewashitua wachambuzi wengi wa kandanda kuona CAF haikumjumuhisha nyota wa Senegal, Ismaila Sarr, ambaye aliipa Crystal Palace taji la Conference League akiwa mfungaji bora [mabao matano] na mchezaji bora wa michuano hiyo.
Wakati huo huo, Sarr aliifungia mabao manne, likiwamo moja dhidi ya Ubelgiji, wakati Senegal ilipofika hatua ya 32 ya fainali zilizopita za Kombe la Dunia.
Kwa mwaka huu, amefunga jumla ya mabao 24 na kutoa asisti tano katika mechi 53 za klabu na timu ya taifa.
Kwa orodha hii ya wachezaji watano, Hakimi wa PSG na timu ya Taifa ya Morocco anapewa nafasi kubwa ya kuwa Mchezaji Bora wa CAF mwaka 2026.
Hakimi aliipa PSG taji la pili mfululizo la Ligi ya Mabingwa Ulaya, wakati huo pia akiiwezesha Morocco kufika robo fainali ya Kombe la Dunia.
Mwenzake kwenye kikosi cha Morocco, Diaz, alimaliza mashindano ya AFCON 2025 akiwa mfungaji bora [mabao matano].
Nyota mwingine wa kikosi hicho, Saibari, alifunga mabao matatu kwenye Kombe la Dunia, ambapo alizitungua Brazil, Scotland na Haiti.
Kwa ufupi, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Afrika kufunga bao katika mechi zote tatu za hatua ya makundi kwenye msimu mmoja wa Kombe la Dunia.


