15.1 C
New York

Rais Trump dhidi ya vyombo vya habari Marekani

Published:

WASHINGTON DC, Marekani

HIVI karibuni, vyombo vya habari vitatu maarufu vya Marekani vilimshitaki mahakamani Rais Donald Trump baada ya kiongozi huyo kuvipiga marufuku kuingia Ikulu.

Vyombo vya habari hivyo ni CNN, Politico na MS NOW, ambavyo kwa mujibu wa Rais Trump vimekuwa vikiripoti habari za uongo [fake news] juu ya utawala wake.

“Waandishi wa habari za uongo ambazo huandika tu kuhusu mabaya na kutishia Usalama wa Taifa kwa habari za uongo zisizo na vyanzo rasmi hawapaswi kusogelea ofisi muhimu kokote pale duniani,” aliandika Trump kupitia ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Truth Social.

Katika utekelezaji wa agizo lake hilo, waandishi wa vyombo hivyo walizuiwa kuingia Ikulu wakati wa hafla ya chakula cha usiku, jambo lililozua mjadala mkubwa.

Hatua hiyo ya kuzuiwa kuingia Ikulu ilikuja wakati tayari Mahakama nchini Marekani ilishamtaka Rais Trump kuachana na katazo hilo kwani linakiuka Katiba ya nchi inayoitaka Serikali kutokuingilia uhuru wa vyombo vya habari.

Baada ya ugomvi wake na CNN, Politico na MS NOW, vyombo vingine vya habari vya ABC, CBS, CNN, Fox News na NBC navyo vilikuja juu kumshambulia Rais Trump.

Kupitia taarifa ya pamoja, vyombo hivyo vilieleza: “Umma unataka kupata taarifa sahihi kuhusu serikali yake. Hakuna uongozi [wea Serikali] wenye nafasi ya kuzuia chombo cha habari kutekeleza majukumu yake ya kuripoti.”

Februari, 2026, uongozi wa Rais Trump ulieleza mpango wake wa kudhibiti vyombo vya habari vinavyofanya kazi na Ikulu. Ni jukumu ambalo kwa miaka mingi limekuwa likifanywa na Chama cha Waandishi wa Ikulu na si Serikali.

Mwezi huo huo, waandishi na wapigapicha wa Shirika la Habari la AP walizuiwa kuingia Ikulu. Ni baada ya chombo hicho kutumia neno lililoonesha kuwa sehemu ya Mexico si ardhi ya Marekani kama anavyodai Rais Trump. AP walifungua kesi mahakamani na bado inaendelea.

Hata hivyo, imekuwa ni kawaida kwa Rais Trump kuingia kwenye vita na baadhi ya vyombo vya habari. Wakati fulani, utawala wake ulivifungulia mashitaka New York Times, Wall Street Journal na hata BBC.

Katika baadhi ya kesi, vyombo hivyo vimejikuta vikikubali kulipa fedha nyingi kama fidia. Mashitaka yake dhidi ya BBC bado yanaendelea kufukuta mahakamani.

Hata hivyo, Rais Trump si kiongozi wa kwanza wa Marekani kuingia kwenye mvutano na vyombo vya habari. Uongozi wa Barrack Obama ulijaribu kuizuia Fox News kushiriki
katika mahojiano na viongozi wa Serikali mwaka 2009. Fox News iliruhusiwa kushiriki baada ya vyombo vingine kupaza sauti.

Related articles

Recent articles