LOS ANGELES, Marekani
MAKALA ya maisha ya mwanamitindo Katie Price imejaa simulizi yenye huzuni juu ya maisha ya bibiye huyo mwenye jina kubwa katika tasnia ya burudani.
Katika makala hayo ya video yaliyopachikwa jina la ‘Katie Price: Nothing to Hide’, Katie mwenye umri wa miaka 48, amefichua mengi, ikiwamo hatua ngumu ya kutaka kujiua.
Pia, Katie amegusia maisha yake na Peter Andre aliyepata naye watoto wawili; Princess (19) na Junior (21).
Watoto hao ni kati ya watano alionao Katie katika mahusiano yake na wanaume watatu tofauti.
Kupitia makala hayo, Princess na Junior pia wanasikika wakisimulia maisha magumu waliyopitia wakati mama yao akiteswa na urahibu wa dawa za kulevya.
Julai, 2023, Katie alifichua kuwa amekutwa na tatizo la ubongo, ambalo kitaalamu linaitwa ADHD, wakati alipokuwa hospitali kwa kwa matibabu ya afya ya akili.
Anakiri kuwa changamoto ya afya ya akili ilitokana na tukio baya la kubakwa na majambazi mwaka 2018 akiwa nchini Afrika Kusini.
Ni baada ya kufanyiwa unyama huo, Katie anasema alitaka kujiua kwa kujinyonga, kabla ya kuachana na wazo hilo baada ya kuwafikiria watoto wake watano.
Tukio hilo lilimfanya ajikute kwenye kiwango kikubwa cha matumizi ya dawa za kulevya aina ya cocaine, pia ulevi wa pombe uliopindukia.
Septemba, 2021, Katie aliingia mikononi mwa polisi baada ya kunaswa akiendesha gari akiwa amelewa.
Wakati huo huo, pia ndinga hilo la bei mbaya aina ya BMW X5 lilikuwa na shida ya kukosa bima.
Anasema ni kupitia tukio hilo, alibaini anahitaji msaada.
Katie anafahamika kuwa ni miongoni mwa wanamitindo waliofanya mara nyingi upasuaji wa kurekebisha muonekano.
Mathalan, katika maisha yake ya kazi ya uanamitindo, amefanya upasuaji mara 17 wa kurekebisha sehemu mbalimbali za miwili, ikiwamo matiti na sura.
Hata hivyo, mama yake aitwaye Amy amewahi kuweka wazi kuwa hajawahi kuvutiwa na tabia hiyo ya binti yake na amekuwa akimwambia hilo mara kwa mara.


